1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaanza maisha vizuri bila ya Toni Kroos na Neuer

9 Septemba 2024

Timu ya taifa ya Ujerumani imeanza maisha bila ya wachezaji nyota wanne waliostaafu, Ilkay Gündogan, Manuel Neuer, Thomas Müller na Toni Kroos kwa mguu mzuri baada ya kuitandika Hungary mabao 5-0 mjini Düsseldorf.

Fußball-EM 2024 | Achtelfinale | Deutschland vs. Dänemark | Jubel 2:0
Jamal Musiala akisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya DenmarkPicha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Jamal Musiala alikuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Hungary kwa kutoa pasi tatu za mabao na yeye mwenyewe kuuweka mpira kambani mara moja.

Ujerumani sasa itachuana na Uholanzi kesho Jumanne katika mechi yao ya pili ya ligi ya mataifa ya Ulaya UEFA Nations League.

Soma pia: Toni Kroos mwanasoka bora wa mwaka wa Ujerumani 

Kuelekea mechi hiyo itakayopigwa katika dimba la Johan Cruijff Arena mjini Amsterdam, kocha Julian Nagelsmann amesema,

"Hatuna kikosi kipya kabisa kwa wakati huu. Kwa kweli haya ni mabadiliko makubwa, tumepoteza wachezaji wanne muhimu na wenye uzoefu. Lakini wachezaji wanajuana, tuna wachezaji wapya. Kikosi kinaonekana kuwa na mshikamano na nadhani hatuhitaji maandalizi makubwa kwa ajili ya mchezo wa kesho."

Kama ilivyokuwa kwa Ujerumani, Uholanzi pia ilianza kampeni yao kwa ushindi wa kishindo kwa kuipiga Bosnia na Herzegovina mabao 5-2, na kuiacha timu hiyo inayotiwa makali na Ronald Koeman ikiwa nyuma ya Ujerumani kwenye msimamo wa kundi A kwa tofauti ya mabao.