Ujerumani yachukizwa na udukuzi wa simu ya Merkel
24 Oktoba 2013Kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, waziri wa mambo ya kigeni, Guido Westerwelle, atakutana ana kwa ana baadaye hii leo mjini Berlin na balozi John Emerson ili kuzungumzia suala hilo lililozua wasiwasi mkubwa nchini Ujerumani.
Habari hizi zimekuja wakati Merkel na viongozi wengine barani Ulaya wanakutana mjini Brussels kwa mkutano ambao unaonekana utagubikwa na habari za mawasiliano ya siri yanayodaiwa kufanywa na Marekani kwa washirika wake.
Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, aliliambia shirika la habari la ARD la hapa Ujerumani iwapo madai haya yatathibitishwa kuwa ya kweli basi litakuwa ni jambo baya sana.
De Maiziere amesema Marekani itabakia kuwa marafiki wa Ujerumani lakini jambo linalodaiwa kufanywa sio sahihi kabisa. Naye kiongozi wa chama cha mrengo wa shoto, Die Linke, Gregor Gysi, amesema matukio ya hujuma kutoka kwa Marekani yanapaswa kusimamishwa na kwamba Marekani sio taifa lenye nguvu linaloimiliki dunia.
Serikali ya Ujerumani imepokea taarifa kwamba Marekani ilifuatilia mawasiliano ya kansela Angela Merkel, hatua iliomfanya Merkel mwenyewe hapo jana Jumatano kumpigia simu mara moja rais wa Marekani, Barack Obama, kutaka ufafanuzi zaidi.
Awali Kansela Merkel alisema alijua mawasiliano yake ya simu labda yangefuatiliwa siku moja lakini hakudhani Marekani ndio itakuwa ikifanya hivyo.
Marekani hata hivyo kupitia msemaji wa ikulu, Jay Carney, imekanusha madai hayo. "Naweza kukwambia kuwa rais Obama amehakikisha Marekani haifuatilii na haitafuatilia mawasiliano ya kansela." Alisema Carney.
Madai makubwa yanayosema Marekani inachunguza mawasiliano ya washirika wake, yalitolewa kwa mara ya kwanza na mfanyakazi wa zamani wa idara ya kitaifa ya usalama nchini Marekani, NSA, Edward Snowden, yaliyochapishwa na jarida la habari la Ujerumani, Der Spigel.
Madai hayo yameanza kuleta uhusiano mbaya kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya yaliyokasirishwa na habari hizo za kufanyiwa uchunguzi wa siri na mshirika wao.
Kwa upande wa magazeti ya hapa Ujerumani kama Die Welt limeitaja habari hii kuwa ya kufedhehesha kwa mashirika ya usalama ya Ujerumani huku gazeti la Sueddeutsche Zeitung likisema hili tusi kubwa kuwahi kufikiriwa kwa Ujerumani.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Josephat Charo