1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yachukua hatua kuzuwia kusambaa virusi vya Corona

Sekione Kitojo
27 Februari 2020

Maafisa wa afya Ujerumani wamechukua hatua ili kupambana na virusi vya Corona nchini humo, wakati idadi ya maambukizi ikipanda kwa  kasi na sekta ya viwanda imeonya kutokea athari kubwa katika uchumi wa nchi hiyo.

Deutschland Uniklinik Düsseldorf | Coronavirus
Picha: Reuters/W. Rattay

Serikali ya  Italia  nayo  ikihangaika  kuzuwia mdororo  wa uchumi, inajitahidi  kupuuzia  hali  mbaya  ya  maambukizi  ya  virusi vya  Corona nchini  humo, ikiwa  ni  nchi pekee  ya  Ulaya  ambayo imeathirika  zaidi. 

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Reuters/M. Tantussi

Watu mia  kadhaa  wamewekwa  chini  ya  karantini  majumbani mwao  katika  jimbo  lenye wakaazi  wengi  la  upande  wa  magharibi mwa  Ujerumani  la  North Rhine  Westfalia  baada  ya  mwalimu wa shule  ya  chekechea , aliyeshiriki  katika  sherehe  za  kitamaduni za  Kanivali , kuthibitishwa  kuwa  ameambukizwa  na  virusi  vya Corona.

Wale  waliwekwa  chini  ya  karantini  wamebakia  majumbani  mwao kwa  siku  14  wakati  marafiki  na  ndugu  wakiwapelekea  mahitaji ya  chakula  na  kadhalika, wakiviweka  vitu  hivyo  nje  mlangoni  na kuepuka  kugusana  nao. takriban  watu  10  wapya  wamethibitishwa kuwa  na  virusi  hivyo  vya  Corona  nchini  Ujerumani, na  msako wa  watu  wengine  walioathirika  umeendelea  leo  Alhamis.

Mkuu  wa  kitengo  cha  nje  katika  halmashauri  ya   viwanda  na biashara  nchini  Ujerumani DIHK, Volker Treier, ametabiri  kwamba uchumi  wa  Ujerumani  utaathirika  sana  katika  mwaka  huu  2020.

Kifuniko cha mdomo na pua kuzuwia mambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona mjini BerlinPicha: Imago Images/photothek/X. Heinl

Idadi ya vifo yapanda

Nchini  Italia,  nchi  ambayo imeathirika  zaidi  katika  mataifa  ya Ulaya, mbali  ya  mawaziri  kutoa  ujumbe  wa  uhakikisho , maafisa wanasema  idadi  ya  vifo  imepanda  kwa  watu  wawili  na  kufikia watu 14 usiku wa  jana, wakati  idadi ya  watu  ambao  wamethibitika kuwa  wameambukizwa  ugonjwa  huo  imepanda  kwa  zaidi  ya watu 100  na  kufikia  watu 528.

"Janga  la  kutoa  taarifa  za  upotoshaji  litaleta  madhara  makubwa zaidi  nchini  Italia  kuliko hatari ya  janga  la  virusi  vyenyewe," waziri  wa  mambo  ya  kigeni Luigi Di Maio alisema  katika  mkutano na  waandishi  habari. Ni  moja  tu  asilimia  ya  nchi  ambayo inahusika  na  ugonjwa  huo,  ameongeza  Di Maio.

Mashirika  ya  habari  ambayo  si  ya  serikali  nchini  Iran yameripoti  kuwa  swala  ya  Ijumaa  imefutwa  mjini  Tehran  na kwingineko  katika jamhuri  hiyo ya  Kiislamu  kuhusiana  na  kuzuka kwa   virusi  hivyo.

Taarifa  hizo  zimejitokeza  leo  wakati  Iran  imekuwa  na  ongezeko la  watu  walioambukizwa  virusi  hivyo kwa  zaidi  ya  watu 100   na kufikisha  watu 254.

Wasafiri wakifunika mdomo na pua kuzuwia maambukizi ya virusi vya CoronaPicha: Getty Images/L. Dray

Wakati  huo  huo nchi hiyo  imechukua  hatua  ya  kupiga  marufuku raia  wa  China  kuingia  nchini  humo, shirika  la  habari la  Iran IRNA limeripoti leo, kutokana  na  kusambaa  kwa  virusi  vya Corona  katika  taifa  hilo.

Saudi Arabia  imesitisha  safari  kwenda  katika  maeneo  takatifu nchini  humo, kwa  watu  kutoka mataifa  yaliyoathirika  zaidi  na virusi  vya  Corona, na  Korea  kusini  imeimarisha  adhabu  kwa wale  watakaokiuka amri  ya  karantini  na  maafisa  wa  viwanja  vya ndege  katika  mataifa  ya  Amerika kusini  wanaangalia  ishara kumtambua  abiria  mgonjwa, wakati  virusi  hivyo  vikiendelea kusambaa  kote  duniani.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW