1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yachukua urais wa muungano wa kanda ya Sahel

Sylvia Mwehozi
10 Julai 2023

Ujerumani imechukua urais wa muungano wa kimataifa wa nchi zinazounga mkono kanda ya Afrika ya Sahel. Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze alihudhuria mkutano mkuu uliofanyika mjini Nouakchott Mauritania .

Niger Niamey | Pistorius na Schulze watembelea kanda ya Sahel
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze(kulia) na waziri wa ulinzi Boris Pistorius(kushoto) walipokuwa Niger mwezi Aprili. Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Ujerumani imechukua urais wa muungano muhimu wa kimataifa wa nchi zinazounga mkono kanda ya Afrika ya Sahel. Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze alihudhuria mkutano mkuu wa muuungano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Mauritania Nouakchott siku ya Jumatatu.

soma pia: Viongozi wa G5 wafanya mkutano kujadili vita dhidi ya ugaidi

"Ninachukua urais wa Muungano wa Sahel ili kuonyesha kwamba Ujerumani, pamoja na washirika wake, ipo na inajitolea kwa ajili ya kanda hii," alisema Schulze. Waziri huyo amebainisha vipaumbele vya Ujerumani wakati wa uongozi wake kuwa ni ajira, kilimo na usalama wa kijamii katika kanda ya Sahel.

Muungano wa Sahel wenye wanachama 18 ulianzishwa mwaka 2017 na Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kusaidia nchi za kundi la nchi za G5 za kanda ya Sahelambazo ni Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad zinazotishiwa na umaskini mkubwa na ugaidi.

Mawaziri wa ulinzi na maendeleo wa Ujerumani Boris Pistorius Svenja Schulze na kiongozi wa kijeshi wa Mali Assimi GoitaPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Hadi kufikia sasa, muungano huo umetumia zaidi ya euro bilioni 30.66 katika kanda hiyo huku Ujerumani ikiwa ni mfadhili wa nne kwa ukubwa nyuma ya Benki ya Dunia, Ufaransa na Umoja wa Ulaya.

Schulze ameelezea kwamba "Sahel ni mojawapo ya kanda maskini zaidi duniani na yenye idadi kubwa ya vijana wadogo. Wakati huo huo, Sahel imekuwa kitovu kipya cha ugaidi wa makundi ya itikadi kali za Kiislamu na ushawishi wa Urusi unaongezeka."

Urais huo wa Ujerumani utajielekeza zaidi katika miradi ya elimu na ajira, upanuzi wa ulinzi wa kijamii na miradi ya kijamii ya usambazaji maji, hospitali, shule na masoko.Merkel yaitolea wito Ulaya kupambana na ugaidi eneo la Sahel

Mataifa yanayozungumza lugha ya Kifaransa ya Sahel yaliunganisha vikosi mwaka 2014 haswa kupambana na wanamgambo wa itikadi kali. Makundi yenye silaha, mengi yakiwa na mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na lile la Al-Qaeda yamekuwa yakidhibiti eneo hilo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Mali, Burkina Faso na Niger ndio nchi zilizoathirika pakubwa. Zaidi ya watu milioni 2.8 wamekimbia makaazi yao, zaidi ya milioni 2 ni wa Burkina Faso.

Chanzo: dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW