Ujerumani yaendelea vyema na safari ya Brazil
13 Oktoba 2012Ushindi mkubwa wa magoli sita kwa sifuri wa Ujerumani dhidi ya Ireland katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za kombe la dunia ulirejesha utulivu ndani ya kikosi hicho, baada ya kushuhudiwa msukosuko tangu ilipoondolewa katika nsusu fainali ya dimba la UEFA EURO 2012 mnamo mwezi Juni.
Kocha Joachim Löw alishutumiwa katika miezi iliyopita kwa kushindwa kukitumia vyema kikosi kilichojaa wachezaji mahiri ambacho hakijapata taji lolote kuu kwa miaka 16.
Rais wa Bayern Munich Uli Hoeness pia alimshutumu Löw kwa kuwa mpole sana kwa wachezaji wake wakati kiungo Bastian Schweinsteiger alipotoa wito wa kuwepo kiwango cha juu cha nidhamu kambini, ili wapige hatua nyingine. Lakini baada ya kusajili ushindi wao wa tatu mfululizo katika mechi za kufuzu kwa kombe la dunia na uwezekano kuzoa pointi zote 12 watakapocheza na Sweden tarehe 16 mwezi huu, timu ya Löw iko katika hali nzuri na inapigiwa upatu kuongoza katika kundi hilo.
Miongoni mwa wachezaji walioisaidia Ujerumani kupata ushindi wa jana ni beki wa kushoto Marcel Schmelzer, ambaye alishutumiwa vikali na kocha Löw kabla ya mchuano huo. Lakini Löw amesema beki huyo anaweza kuimarika na kucheza vyema jinsi anavyofanya katika klabu yake ya Borussia Dortmund.
Miroslav Klose pia alionyesha mchezo mzuri na kufunga goli, wakati akijaribu kuifikia rekodi ya mfungaji bora wa Ujerumani Gerd Mueller ya mabao 68. Huku Sweden wakiwa wageni wa Ujerumani mjini Berlin wiki ijayo, wenyeji wao wanataraji kuwa watawafurahisha mashabiki wa nyumbani, katika juhudi zao za kujaribu kulifikia kombe la dunia nchini Brazil katika miaka miwili ijayo.
Wanariadha wa Kenya walalamika kuhusu kodi
Tukiachana na kandanda sasa tuangalie riadha ambapo anayeshikilia rekodi ya Olimpiki na Ulimwengu katika mbio za mita 800 David Rudisha na bingwa wa ulimwengu wa mita 10,000 na 5,000 Vivian Cheruyiot ni miongoni mwa kundi la wanariadha wa Kenya wanaopinga mpango wa kukatwa kodi pesa zao wanazopata baada ya mashindano.
Cheruyiot anasema hivyo siyo vyema. Anasema wao hutumia pesa zao nyingi katika kuchangia uchumi wa Kenya. Anaongeza kusema kuwa wao hupeleka pesa nchini mwao na kuwekeza katika miradi mbali mbali ambayo tayari hutozwa kodi kubwa sana.
Wanariadha hao walipokea barua kutoka kwa Mamlaka ya kukusanya kodi KRA, ambazo ziliwataka walipe kodi za mapato yao ya mashindano ya kigeni. KRA ilisema inawalenga tu wanaridha ambao wamelipa kodi ya chini ya asilimia 30 katika nchi ambazo wameshinda pesa hizo, lakini baadhi ya wanariadha wanasema wametakiwa kulipa kiasi kikubwa cha pesa kama malimbikizi ya kodi. Wanariadha hao wanatarajiwa kukutana na Chama cha Riadha cha Kenya ili kujadili suala hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri : Mohamed Dahman