Ujerumani yaidhinisha ndoa za jinsia moja
30 Juni 2017"Kwangu mimi ndoa katika Sheria ya Msingi ni ndoa kati ya mwanaume na mwanamke na ndio sababu sikupiga kura ya kuunga mkono muswada huu leo hii.Ni kweli hicho kilichosemwa katika mdahalo wa leo. Ulikuwa ni mdahalo uliochukuwa muda mrefu ni mzito na kwa wengi yalikuwa majadiliano yenye hisia nzito.Jambo hili pili limenigusa mimi mwenyewe binafsi.Ndio sababu natumai kura hii leo hii sio tu inakuza heshima baina ya maoni tofauti bali pia inaleta maelewano zaidi ya kijamii na amani.Asante."
Kauli hiyo ameitowa Merkel anayewania muhula wa nne madarakani katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Septemba 24 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya uamuzi huo wa kihistoria ulioidhinisha ndoa ya watu wa jinsia moja nchini Ujerumani ambapo binafsi amepiga kura ya kuukataa kwa sababu anaamini kwamba ndoa ni kama inavyoelezewa na sheria ya Ujerumani ni kati ya mwanaume na mwanamke.
Lakini amesema uamuzi wake huo ni wa binafsi na kuongeza kwamba amezidi kupata imani miaka ya hivi karibuni kwamba wana ndoa wa jinsia moja wanapaswa kuruhusiwa kusaili watoto.
Kura 393 zaunga mkono didi ya 226
Nobert Lambert Spika wa bunge la Ujerumani amesema wabunge 393 wamepiga kura ya kuunga mkono ndoa ya jinsia moja wakati wabuge 226 wamepiga kura ya kupinga na wabunge wanne hawakupiga kura.
Nchi nyengine nyingi za Ulaya ikiwemo Ufaransa,Uingereza na Uhispania tayari zimehalalisha ndoa za jinsia moja.
Tangazo la Merkel alilolitowa hapo Jumatatu kwamba atawaruhusu wabunge kupiga kura juu ya ndoa ya jinsia moja kwa kuzingatia imani zao binafsi limewakera baadhi ya wabunge wanaounda muungano wake wa kihafidhina ambao kwa jadi umekuwa chini ya msingi wa Kikatoliki.
SPD yauona huo ni ushindi kwao
Kura hii ya leo inaadhimisha ushindi wa nadra kwa chama cha Social Demokrat (SPD) ambacho ni mshirika wa Merkel katika serikali yake ya mseto ambacho kiko nyuma ya wahafidhina kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni.
Thomas Opperman mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha SPD bungeni amesema
"Kwamba leo tunaamuwa tu pengine sio kitu kizuri kwa serikali ya mseto lakini ni jambo zuri kwa wananchi."
Chama hicho cha SPD kimetumia fursa ya tamko la kushangaza la Merkel alilolitowa Jumatatu kwao wao kusema kwamba watashinikiza kupigwa na mapema kwa kura hiyo ya kuidhinisha ndoa za jinsia moja nchini Ujerumani.
Lakini wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba suala hilo yumkini litakuwa limefifia kwenye mawazo ya wapiga kura utakapofika wakati wa uchaguzi mkuu hapo mwezi wa Septemba.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mwandishi: Yusuf Saumu