1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaomba msamaha kutokana na vita vya pili vya dunia

1 Septemba 2019

Rais Frank Walter-Steinmeier ameinamisha kichwa chini mbele ya wahanga wa Wielun na kuomba msamaha kwa mauaji yaliyofanywa na Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia chini ya utawala wa Wanazi

Polen Wielun Gedenken an den Beginn des 2. Weltkrieges mit Bundespräsident Steinmeier
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

 Marais wa Ujerumani na Poland wamefungua maadhimisho ya siku nzima ya kumbukumbu za miaka 80 tangu vilipoanza vita vya pili vya dunia kwa sherehe zilizojaa imani ya maridhiano na huruma ya Wajerumani kutokana na mateso yaliyosababishwa wakati wa vita hivyo.

 Maadhimisho hayo yamefanyika katika mji wa Wielun,mji ulioko katikati mwa Poland ambao ulikuwa ni wa kwanza kulengwa na mashambulizi ya vikosi vya utawala wa Wanazi wa Ujerumani.

Ujerumani yaomba msamaha

Rais Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa Poland Andrzej Duda wamehudhuria maadhimisho hayo yaliyoanza saa kumi na dakika arubaini za alfajiri muda kamili wa tukio la kudondoshwa mabomu kwa mujibu wa walionusurika katika mashambulizi hayo ya mabomu ya mwanzo kabisa yaliyouwa raia.

Marais,viongozi wa eneo hilo,pamoja na wakaazi miongoni mwao wakiwemo walionusurika wakati huo walikaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga takriban 2,000. Rais wa Ujerumani Steinmeier amezungumza kwa lugha ya Kijerumani na Kipoland kuomba msamaha,akisema na hapa tunanukuu.

Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

'' Nainamisha kichwa changu mbele ya wahanga wa shambulio la Wielun,Nainamisha kichwa changu mbele ya wahanga wa Poland katika mashambulizi yaliyofanywa na Ujerumani na naomba msamaha''

Alisema pia kwamba Ujerumani inashukuru kwa Poland kunyoosha mkono wa kusamehe. Kadhalika ameahidi kama rais wa Ujerumani kwamba nchi yake haitosahau bali itakumbuka kila siku kuhusu tukio hili na wanataka kulikumbuka na kuchukua dhamana kwamba historia yao inawalazimu.

Rais wa Poland amemshukuru Steinmeier kwa kuhudhuria kumbukumbu hizo zinazoleta uchungu na kusema ni njia inayotoa mtazamo wa kuridhisha kimaadili. Dakika kadhaa baadae waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki na afisa wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya Frans Timmermans  waliwaongoza washiriki katika rasi ya Westerplatte kwenye  pwani ya Baltic ambako ndiko mapigano ya mwanzo yalikotokea wakati wanajeshi wa Poland walipoimarisha upinzani.

Maadhimisho kamili

Na mchana leo Jumapili makamu wa rais wa Marekani Mike Pence,Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pamoja na kiongozi wa chama tawala nchini Poland Jaroslaw Kazcynski wataungana na Steinmeier na Duda na viongozi wengine wengi katika tukio kamili la maadhimisho ya kumbukumbu hizo mjini Warsaw.

Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Ikumbukwe kwamba kuvamiwa kwa Poland na wanajeshi wa utawala wa wanazi Septemba Mosi mwaka 1939 ndiko kulikosababisha kuzuka kwa vita vya pili vya dunia.

Kitisho cha vita hivyo bado kinaonekana hadi wakati huu ambapo takriban wakaazi 3,000  walilazimika kuhamishwa katika mji wa Magharibi wa Boleslawiec kutoa nafasi ya wataalamu wakijeshi kuondowa makombora 37 ambayo hayakulipuka wakati wa vita. Leo hii Ujerumani na Poland ni washirika katika Jumuiya ya Nato na Umojá wa Ulaya na zina ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na kibiashara.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Tatu Karema