Ujerumani yaipa Tanzania bilioni 78 kusaidia miradi ya maji
16 Julai 2025
Miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kunufaika na msaada huo ni ya kwenye hifadhi za taifa za Serengeti na Katavi ambako uboreshaji wa miundombinu, utoaji elimu pamoja na kuendeleza miradi ya kijamii inayozunguka hifadhi hizo ni sehemu ya vipaumbele vya msaada huo uliotolewa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).
Katika eneo la hifadhi ya taifa, utawezesha wataalamu katika maeneo hayo kupata mbinu na uwezo mpya wa kuendeleza utalii na uhifadhi ili kufanya shughuli zote zinazofanywa kwenye maeneo hayo kuwa endelevu.
Nuhu Daniel, ambaye ni msaidizi wa uhifadhi Tanapa, anasema suala la uboreshaji wa barabara ndani ya maeneo ya hifadhi ili kuziwezesha kuwa na uwezo wa kupitika katika kipindi chote cha mwaka ni eneo lingine ambalo limezingatiwa na fedha za msaada huo.
Vikundi vya maendeleo kunufaika na msaada wa Ujerumani
Vikundi ya maaendeleo pamoja na shughuli za kijamii zinazoendeshwa na wakazi wanaishi kandokando na maeneo ya hifadhi watasaidiwa kwa kupatiwa mikopo kupitia vikundi vyao vinavyofahamika kama benki za maendeo ya kijamii.
Michael Gikaro ambaye ni mwenyekiti wa mmoja ya vikundi vilivyopo karibu ya eneo la hifadhi anasema mikopo wanayopatiwa imewawezesha kuendesha familia kwa kuanzisha biashara, kupeleka watoto shule na hata kupata matibabu.
Hivi karibuni serikali ya Ujerumani ilitoa mafungu ya fedha ili kufadhili usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria na kuwafikia wakazi wa maeneo ya kanda ya ziwa waliokuwa wakikabiliwa na adha ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu.
Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Manuel Meuller, anasema shabaha ya mradi huo ni kuziwezesha kaya zaidi katika eneo hilo kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Serikali ya Tanzania inasema mamlaka za maji zimefunguliwa milango kuanzisha miradi ya uendelezaji huduma ya maji, na kulingana na katibu mkuu wizara ya fedha, Dk Natu El-maamry Mwamba mamlaka hizo sasa zinaweza kukopa kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya maji.
Tanzania imekuwa katika kampeni ya kile kinachojulikana "kumtua mama ndoo kichwani" ikimaanisha kumaliza kabisa adha ya ukosefu wa maji ambayo mara nyingi mzigo wake hubebwa na wanawake.