1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaisaidia Rwanda kupata nishati endelevu

Admin.WagnerD10 Januari 2011

Afrika ina uhaba wa nishati; ambapo chanzo kikubwa cha nishati kinachotumika ni kuni ambazo huhatarisha mazingira kutokana na ukataji miti; lakini si kwa kuwa Afrika haina nishati nyengine mbadala. La hasha!

Ziwa Kivu, Rwanda
Ziwa Kivu, RwandaPicha: DW / Irene Anastassopoulou

Hivi sasa, mradi wa Kijerumani wa ulinzi wa mazingira, unasaidiana na jamii ya Kinyaruanda katika kutafuta suluhu la nishati kupitia vyanzo vya nishati mbadala.

Alex Kabuto ni mhandisi anayejihusisha na mradi wa uzalishaji wa methani, ambayo ni gesi inayopatikana karibu na maziwa, mito, milima au hata bahari. Rwanda ni nchi ambayo haina bahari, lakini moja kati ya maziwa makubwa barani Afrika, Ziwa Kivu, liko mpakani mwa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hivi sasa kunaendelea mradi mkubwa wa kuzalisha gesi ya methani kutoka ziwa hilo, unaosaidiwa na kampuni ya Kijerumani.

Akiwa kwenye chumba chake kidogo chenye kompyuta, inayoendesha mtambo wa kusafisha methani, ili iwe tayari kwa ajili ya kutumika kwa nishati, Kabuto anasema kwamba, uamuzi wa serikali ya Rwanda kutumia gesi hii, ili kuepukana na matumizi ya nishati za mafuta ya petroli zinazoathiri mazingira, una faida kubwa.

"Serikali iliamua kuitoa gesi iliyomo kwenye ziwa. Kiwango kikubwa cha gesi kama hiki kikiachiwa bila kuchimbwa ni hatari, maana kimeshakaa ardhini kwa zaidi ya miaka mia moja hadi mia tano. Kuna mifano kama hiyo imetokea Cameroon, ambako gesi iliripuka na watu na wanyama wengi wakafa." Anasema Kabuto.

Gesi kama hii ndiyo iliyomo kwenye mivungu ya milima ya Volkano, ambayo ina kiwango kikubwa cha nishati, ambacho ni salama kutumika kama kitachimbwa kidogo kidogo, lakini ni hatari sana kama itawachwa kuripuka wenyewe.

Baada ya gesi kukusanywa kwenye kituo anachofanyia kazi Kabuto, husafirishwa kupitia mabomba makubwa ya usafirishaji kwenda kwenye viwanda vya uzalishaji umeme, na huko huingia kwenye vinu vya umeme, vilivyotengenezwa hapa Ujerumani, ambako kiasi cha megawati 3.6 za umeme huzalishwa. Na huu ni mpango wa majaribio tu, maana kwa uhakika, methani inaweza kuzalisha zaidi ya kiwango hicho cha umeme.

"Gesi kutoka Ziwa Kivu inaweza kuzalisha hadi megawati 700, ambazo ni zaidi ya mahitaji ya Rwanda. Lengo letu ni kuzalisha umeme mwingi kadiri inavyowezekana ili mwengine tuweze kuuza nje. Rwanda inaweza kuwa kivutio cha uwekezaji tutakapokuwa na umeme wa kutosha na ambao pia ni rahisi." Anasema Kabuto.

Usafirishaji wa bidhaa kupitia Ziwa KivuPicha: DW/Anastassopoulou

Mjini Kigali watu wanausubiri kwa hamu muda huo ufike. Serikali yao ina mpango mzuri na wa muda mrefu wa kuifanya nchi kuwa kivutio kwa wawekezaji. Lakini kwa sasa, wanajikuta wanatumia zaidi ya asilimia kumi ya pato lao kuwashia taa tu majumbani mwao. Sababu ni kuwa nchi ina uhaba wa vyanzo vya nishati. Megawati 11 tu ndizo wanazozipata kutoka vinu vinavyozalisha umeme kwa maji, sehemu iliyobakia inatokana na mafuta ya dizeli wanayoingiza kutoka nje, ambayo kwanza ni ghali na pili yanaharibu sana mazingira.

Lakini ukiwacha hilo la gesi ya methani kutoka Ziwa Kivu, kwa ujumla bara la Afrika limejaaliwa na jua la kutosha, ambalo ni chanzo cha uhakika na cha salama kuliko vyote kwa nishati.

Mtaalamu wa mazingira, Anthony Simm anaamini kwamba kuna siku moja, Afrika kwa kushirikiana na ulimwengu, itauona umuhimu na ulazima wa kutumia rasilimali yake hii, kama inavyoelekea saa hizi katika mfano wa Rwanda.

"Sasa jukumu liko kwa kiwanda mjini Mainz. Kuna viwanda katika eneo la mto Rhine ambavyo vina ushirikiano wa muda mrefu na Rwanda. Tangu mwaka 2004, wazo lilikuwa ni kuwa na gridi moja kubwa kwa ajili ya Afrika ya Mashariki nzima." Anamalizia Simm.

Mwandishi: Simone Schlindwein/ZPR/Mohammed Khelef

Mhariri: Josephat Charo