1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaishutumu Marekani kwa vikwazo vya mradi wa gesi

Sekione Kitojo
21 Desemba 2019

Ujerumani imeishutumu Marekani kwa kuingilia masuala yake ya ndani katika matamshi ya hasira  kuhusiana na uamuzi wa Marekani kuweka vikwazo dhidi ya makampuni yanayohusika na mradi wa kusambaza gesi ya Urusi 

USA/Deutschland Sanktionen gegen Nord Stream 2
Picha: picture-alliance/dpa/B. Wüstneck

Urusi  na  Umoja  wa  Ulaya  pia zimetoa taarifa  zinazokosoa vikwazo  hivyo, siku  moja  baada  ya  rais  wa  Marekani Donald Trump  kutia  saini  kuwa  sheria  hatua  ya  kuzuwia  mali  na upatikanaji  wa  visa  kwa  wale  wanaohusika  katika  mradi  huo  wa Nord Stream 2.

Meli ya kutandika bomba la mradi wa Nord Stream 2 ikiwa kazini katika bahari ya BaltikiPicha: picture alliance/dpa/B. Wüsteneck

Wabunge  wa  Marekani wanataka kuzuwia  kile  wanachokiona kuwa  ni  ongezeko la  utegemezi wa  nishati  kutoka  Urusi  katika mataifa  ya  Ulaya  magharibi kwa  kulenga mradi  huo, ambao  una lengo  la  kuongeza  maradufu usambazaji wa  gesi  asilia  kutoka Urusi  nchini  Ujerumani  kupitia  katika  bomba  lililowekwa  chini  ya bahari ya  Baltiki.

Vikwazo  hivyo  vinalenga  wakandarasi wanaofanyakazi  katika kutandika  bomba  hilo  la  Nord Stream 2, mradi  wenye  thamani  ya euro  bilioni 10 unaotarajiwa  kukamilika  mapema  mwaka  2020, na mradi  mwingine  wa  gesi  wa  Urusi , unaojulikana  kama TurkStream.

Katika  ishara  ya  kwanza  kwamba  vikwazo  hivyo  vinaanza kuuma, mkandarasi  kutoka  Uswisi Allseas imesitisha  shughuli  zake katika  mradi  huo  wa  Nord Stream 2 wakati ikisubiri  maelezo kutoka  maafisa  wa  Marekani  kuhusiana  na  vipengee vya  hatua hizo.

Licha  ya  kuwa  bunge  la  Marekani waliunga  mkono  kwa  kiasi kikubwa  vikwazo, kulikuwa  na  baadhi  wamekosoa  hatua  hiyo ambayo  kimsingi  inawaadhibu  washirika  wa  NATO  kama Ujerumani.

Utandikaji wa bomba la Nord Stream 2 katika bahari ya BaltikiPicha: Reuters/V. Vaganov

Wakati msemaji  wa  Umoja  wa  Ulaya  amekosoa kile  alichokiita "uwekaji  wa  vikwazo dhidi  ya  makampuni  ya  Umoja  wa  Ulaya yanayofanyakazi  halali", serikali  ya  Ujerumani  imesema  Berlin inakataa "aina hii  ya  vikwazo dhidi  ya mataifa  ya  kanda".

Athari kwa makapuni ya Ulaya

"Hatua hii  itayaathiri   makampuni  ya  Ujerumani  na  Umoja  wa Ulaya  na  kufikia  katika  uingiliaji  wa  masuala  yetu  ya  ndani," amesema  msemaji  wa  kansela  Angela  Merkel , Ulrike Demmer.

Msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Urusi  Maria Zakharova  ameishutumu  Marekani  kwa  kuendeleza  nadharia ambazo  zinazuwia  biashara  ya  dunia, na  kuongeza  katika ukurasa  wake  wa  Facebook: "Hivi  karibuni  watadai  kuwa  tuache kupumua."

Lakini Marekani  sio taifa  pekee  kuhoji kuhusu  mradi  huo, Ukraine , Poland  na  baadhi  ya  mataifa  ya  eneo  la  Baltiki pia  yameeleza shaka  yao.

Ukraine  imekuwa  na  wasi  wasi  kuwa  bomba  hilo  jipya litaiondoa  katika  biashara  ya  gesi  na  kuruhusu urusi  kuongeza mbinyo kuhusiana  na  masuala  mengine.

Kibonzo kinachoonesha rais Trump akikataa mradi wa bomba la Nord Stream 2 kutoka Urusi kwenda Ujerumani

Wabunge  wa  Marekani  wameeleza  kuiunga  mkono  Ukraine kama sehemu ya   hatua  yake  hiyo  ya  kisheria  ya  kuweka  vikwazo.

Halmashauri  ya  Umoja wa  Ulaya  imesema  jana  Jumamosi kwamba  inachunguza  athari  za  vikwazo  vya  Marekani  dhidi  ya makampuni  ya  Umoja  wa  Ulaya yanayohusika  katika  ujenzi wa bomba  la  Nord Stream 2 chini  ya  bahari  ya  Baltiki.

Kama  suala  la  msingi, Umoja  wa  Ulaya  unapinga  uwekaji  wa vikwazo  dhidi  ya  makampuni  ya  Umoja  huo  yanayofanya  kazi halali," amesema  msemaji  wa  halmashauri  hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW