Ujerumani yajadili kutuma silaha Iraq
18 Agosti 2014´Mhariri wa gazeti Der Tagesspiegel anasema: "Hakuna suluhu ya kuridhisha pande zote katika mgogoro huu. Mwishoni Ujerumani itabidi iangalie uamuzi gani utakaoleta athari chache zaidi. Baada ya wanasiasa kujadiliana kwa wiki nzima, sasa inaonekana kuwa wengi wako tayari kutuma silaha kwa Wakurdi. Muda wa majadiliano umekwisha. Huu ni wakati wa vitendo."
Gazeti la Schleswig-Holstein am Sonntag linaonya kuwa silaha zitakazotumwa Iraq huenda zisiwafikie Wakurdi na badala yake kutumiwa na waasi wa kundi la IS. Mhariri wa Gazeti hilo hata hivyo anasema "Kwa upande mwingine, mazungumzo peke yake hayatoshi kuutatua mzozo huu. Na hata misaada ya kibinadamu inasaidia kwa kiasi tu kupunguza taabu ya Wairaq. Ujerumani lazima ichukue hatua."
Mhariri wa Gazeti la Nürnberger Nachrichten anaangazia suala la kuuwawa kwa mamia ya watu wa madhehebu ya Yazidi. Mhariri huyo anashangaa kwa nini hakuna nchi inayouoendea Umoja wa Mataifa kudai umoja huo uzuie mauaji ya halaiki yanayoendelea Iraq. Badala yake, Waingereza wanataka kutuma silaha, na Wajerumani wanajadili kuhusu hatua hiyo huku Wamarekani wakifanya mashambulizi ya angani. Mhariri huyu anamalizia kwa kuishauri Ujerumani ipate kibali cha Umoja wa Mataifa kwanza na baada ya hapo ndiyo iangalie uwezekano wa kutuma silaha.
Shughuli za ujasusi
Mada nyingine iliyopewa kipaumbele na wahariri hapa Ujerumani ni kashfa mpya inayohusisha shirika la ujasusi la hapa Ujerumani. Shirika hilo linashutumiwa kusikiliza mazungumzo ya simu ya wanasiasa wa Uturuki kama vile waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan.
Gazeti la Münchener Merkur linakumbusha kwamba kazi ya mashirika ya kijasusi si kufuatilia masuala yanayoonekana wazi wazi, bali kutafuta taarifa za ndani na wakati mwingine hata kuvunja sheria ili kupata taarifa hizo. Bila kufanya hivyo, mashirika ya kijasusi hayana faida yoyote ile.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Inlandspresse
Mhariri: Saumu Yusuf