Ujerumani yajadili kuwarejesha makwao wakimbizi wahalifu
14 Januari 2016Mapendekezo hayo yanatokana na kikao cha bunge hapo jana kilichoitishwa kufuatia mashambulizi ya unyanyasaji na kuwadhalilisha kingono wanawake yaliyotokea mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne.
Iwapo sheria itafanyiwa marekebisho, itakuwa rahisi kuwarejesha makwao wakimbizi na wahamiaji wanaokutikana na makosa ya kufanya uhalifu nchini Ujerumani.
Wahamiaji watakaorejeshwa katika nchi zao ni wale watakaofanya visa vya uhalifu kama kuwajeruhi watu, ubakaji na udhalilishaji wa kingono. Wale watakaohukumiwa vifungo vya zaidi ya mwaka mmoja pia watakuwa katika hatari ya kurejeshwa makwao.
Nchi za kaskazini mwa Afrika zamulikwa
Katibu mkuu wa CSU Andreas Scheuer amezitaka nchi za Kaskazini mwa Afrika kama Morocco na Algeria kuorodheshwa kama nchi salama na hivyo raia wa nchi hizo wanaotafuta hifadhi Ujerumani wanaweza kurejeshwa nchini mwao. Merkel anaunga mkono mapendekezo hayo.
Licha ya kuwa CDU na CSU ambavyo ni washirika wakuu katika serikali ya muungano na chama cha Social Democrats SPD, vinatafautiana na upande wa upinzani kuhusu mapendekezo hayo ya kurejeshwa makwao kwa wakimbizi, vyama vyote vimetaka kuwepo kwa sheria madhubuti kuhusu kushughulikia visa vya udhalilishaji wa kingono na kuwalinda zaidi waathiriwa.
Kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke, Bibi Katja Kipping amewashutumu wabunge kwa kutuama tu katika kuujadili mjadala huo kwa kuwaangazia wahamiaji na kusema kukandamizwa kwa wanawake ni jambo linalofanywa na watu wa kutoka matabaka mbali mbali yakiwemo mataifa ya magharibi.
Kiongozi wa chama cha kijani bungeni Katrin Goering Eckardt pia amemshutumu waziri wa sheria Heiko Maas kwa kupuuzilia mbali pendekezo la chama hicho mwaka jana kufanyia marekebisho sheria ya kushuhgulikia visa vya udhalilishaji kingono akilitaja pendekezo hilo wakati huo kuwa halina maana.
Wasiwasi umeibuka nchini Ujerumani kuhusu jinsi wakimbizi na wahamiaji wanavyojiendesha baada ya mashambulizi ya kingono ya Cologne ambapo polisi imesema imepokea malalamiko zaidi ya mia tano.
Visa hivyo vya uvunjifu wa sheria vimechochea kuongezeka kwa uhasama dhidi ya wageni kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kushoto kama PEGIDA ambalo linapinga wageni.
Wakati huo huo, Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani inahofia kuwa kuna njama ya kufanywa mashambulizi makubwa ya kigaidi kama yale yaliyofanyika mjini Paris, Ufaransa mwezi Novemba mwaka jana.
Chuki dhidi ya wageni yaongezeka
Gazeti la Bild limeripoti kuwa taarifa za siri za kiusalama zinaeleza kuwa shambulizi linaweza kutokea wakati wowote na kuonya kuwa taasisi za serikali, wafanyakazi wa umma pamoja na raia huenda wakalengwa katika mashambulizi hayo.
Hayo yanakuja huku raia wanne wa Ujerumani wakishitakiwa kwa kuunda kikundi cha kigaidi kinacholenga kuwashambulia wakimbizi nchini humu. Waendesha mashitaka mjini Munich wametangaza jana kuwa kikundi hicho kijulikanacho Old School Society kinadaiwa kupanga mashambulizi ya bomu dhidi ya makaazi ya wakimbizi.
Wanaume watatu na mwanamke mmoja wameshitakiwa kwa kuliunda kundi hilo la kigaidi. Watuhumiwa hao walio kati ya umri wa miaka 23 hadi 57 wanadaiwa kukutana kwa mara ya kwanza mwezi Novemba mwaka 2014 ili kujadili jinsi ya kutengeza mabomu na namna ya kuwashambulia wafuasi wa itikadi kali ya Kiislamu wa kundi la Salafi na wahamiaji.
Wakati walipokamatwa mwezi Mei mwaka jana, washukiwa hao wanne walikuwa wameshapanga mipango madhubuti ya kufanya shambulizi la bomu dhidi ya makaazi ya wakimbizi.
Maafisa wa usalama wamesema kumekuweko na ongezeko la wanachama wa makundi ya mrengo wa kulia nchini Ujerumani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wanaowalenga na kuwaandama wakimbizi na wahamiaji, hali inayozidisha hisia za chuki dhidi ya wageni.
Mwandishi: Caro Robi/dw English
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman