Ujerumani yajiandaa kuumana na Slovakia
24 Juni 2016Nahodha Bastian Schweinsteiger amefikia kiwango bora cha mazoezi kinachoweza kumpa fursa ya kuanza mtanange huo wa hatua ya mchujo. Boateng aliondolewa uwanjani katika dakika ya 76 wakati wa mchuano wa Jumanne iliyopita dhidi ya Ireland ya Kaskazini kutokana na maumivu ya musuli wa shavu la mguu. Marcus Sorg ni kocha msaidizi wa timu ya taifa na hapa anaelezea hali ya Boateng "Maumivu sasa yanapungua. Matabibu wanajitahidi sana. Sote tuko na matumaini makubwa. Mimi sio nabii. Lakini tunatumai kuwa itawezekana na sote tunahisi atakuwa shwari"
Hata hivyo, kocha Joachim Loew huenda asifanye maamuzi yoyote ya hatari, ikizingatiwa kuwa kama Ujerumani watashinda wataweza kukutana na timu kama vile mabingwa watetezi Uhispania au Italia, na wenyeji Ufaransa au England katika duru zijazo. Naibu kocha Thomas Schneider anasema kichapo cha mwezi jana cha mabao matatu kwa moja katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Slovakia sio kitu cha kuwapa hofu. "Naamini kuwa mtu hapaswi kutumia mchuano wetu wa kirafiki kuwa ni kipimo. Sasa tuko hatua ya mchujo na tuna wapinzani tofauti kabisa. Wanacheza kiufundi zaidi na wana safu imara ya ulinzi. Tayari wameonyesha hilo kwa sehemu katika dimba hili. Kwetu sisi ni kibarua kikali lakini kibarua tunachoweza kushinda na tutafanya hivyo".
Zella: Ujerumani itatinga robo fainali
Lakini wewe unahisi nani atashinda mechi hii? Bila shaka unamkumbuka marehemu Pweza Paul aliyetabiri matokeo ya Kombe la Dunia, na sasa Zella, tembo mwenye umri wa miaka 49 katika bustani ya wanyama ya Wilhelma mjini Stuttgart hapa Ujerumani ametoa utabiri wake. Anasema Ujerumani itatinga robo fainali ya Euro 2016.
Zella aliuchagua mpira wa Ujerumani badala ya mpira wa Slovakia. Thomas Koelpin ni mkurugenzi wa bustani ya Wilhelma "Zella ana utabiri wa kuvutia sana. Ametabiri Ujerumani itatinga robo fainali kwa kuilaza Slovakia. Wenyeji Ufaransa, mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu, pia itafuzu kwa kuipiku Ireland. Kisha utabiri wa kushangaza ni kuwa Iceland itamwangusha England. Hivyo basi utabiri wake huo unaongeza mvuto katika mechi hizi.
Itabidi tusubiri matokeo ya utabiri wa Zella, lakini tunachofahamu ni kuwa Ireland ina fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya wenyeji Ufaransa. Mchuano huo wa mjini Lyon bila shaka utafufua kumbukumbu za Novemba 18, 2009, wakati Therry Henry alifunga bao kwa kutumia mkono na kuioa tikiti timu yake kucheza katika Kombe la Dunia badala ya Ireland. Katika mtanange mwingine, Ubelgiji itakwaruzana na Hungary.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu