Ujerumani yakumbwa na mgawanyiko kuhusu chama cha AfD
12 Mei 2025
Je,chama cha Alternative für Deutschland (AfD) ni cha mrengo mkali wa kulia au la? Idara ya Ujasusi wa Ndani ya Ujerumani, yaani Ofisi ya Kulinda Katiba, hivi karibuni ilikitaja kuwa "chama cha mrengo wa kulia wa kupindukia kilichothibitishwa.”
Hata hivyo, AfD imefikisha suala hilo mahakamani, na kwa sasa ofisi hiyo ya ujasusi imesitisha matumizi ya kauli hiyo hadi uamuzi utakapofanywa. Ingawa ni kawaida kwa mashauri yanayosubiriwa, AfD inaona usitishaji huo kama ushindi.
Wajerumani wengi wanakubaliana kuwa ajenda ya AfD inapingana na demokrasia, utawala wa sheria na heshima ya utu. Lakini namna bora ya kukabiliana na chama hicho sasa imekuwa suala linaloweza kuongeza mgawanyiko wa kijamii nchini.
Swali moja nyeti hasa kwa serikali mpya inayoongozwa na Kansela Friedrich Merz ni: Je, Mahakama ya Katiba ya Shirikisho inapaswa kufikiria kuipiga marufuku AfD?
Wapinzani wa wazo hilo wanasema hatua hiyo itaongeza mgawanyiko wa kijamii na kwamba wapiga kura milioni 10 wa AfD hawawezi tu kutoweka. Lakini wanaounga mkono marufuku hiyo wanasisitiza kuwa maadui wa demokrasia hawapaswi kuachiwa nafasi ya kuiangamiza.
Johannes Kiess, Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Demokrasia ya Else Frenkel-Brunswik katika Chuo Kikuu cha Leipzig, anaamini kuwa ombi la kuipiga marufuku AfD linapaswa kuchunguzwa.
"Ikiwa itahitimisha kuwa AfD haitishii utaratibu wa kidemokrasia wa msingi, basi tutalazimika kuendelea kushughulika nayo bungeni,” Kiess aliiambia DW.
"Lakini iwapo matokeo yataonyesha kuwa chama hiki kweli ni tishio, basi tutaendelea kuwa na mgawanyiko wa kijamii, lakini angalau hatutakuwa tena na mhusika anayelikuza kwa makusudi.”
Wanahabari wakosolewa kuhusu namna ya kuripoti kuhusu AfD
Tathmini ya awali ya AfD na Ofisi ya Kulinda Katiba pia imeibua mjadala kuhusu jinsi vyombo vya habari vinavyopaswa kuripoti kuhusu chama hicho kwa siku zijazo. Chama cha Waandishi wa Habari wa Ujerumani (DJV) kimewataka wanahabari kubadilisha mbinu zao na kuweka wazi kuwa AfD si chama cha kawaida kutoka safu ya kidemokrasia.
Soma pia: Ujerumani yasitisha lebo ya itikadi kali dhidi ya AfD
Josef Holnburger, Mkurugenzi wa Taasisi ya CeMAS (Center for Monitoring, Analysis and Strategy), anaamini waandishi wa habari wanapaswa kubadilisha namna wanavyoripoti kuhusu AfD. Anarejelea kampeni ya uchaguzi mkuu mwanzoni mwa mwaka ambapo mada ya uhamiaji ilipewa uzito mkubwa ikilinganishwa na masuala mengine, licha ya AfD kudai kuwa hoja zake hazipewi nafasi na vyombo vya habari.
"Lakini AfD haitaridhika kamwe na namna inavyoripotiwa. Ndiyo maana si msaada kuendelea kushughulikia mada zao kwa matumaini ya kuwahamasisha wafuasi wao. Chama hiki kitaendelea kujiona waathirika na kudai kuwa hoja zao zinapotoshwa — hata kama kipaza sauti kiko kila mara mbele yao,” alisema.
Je, kushindwa kwa Merz kwenye uchaguzi wa kwanza wa kansela kutainufaisha AfD?
Holnburger anaonya dhidi ya kuiinua AfD kupita kiasi, na kuongeza kuwa kushindwa kwa Merz kwenye duru ya kwanza ya kura kunatoa picha ya kutojiamini. Jumanne, Merz alishindwa kupata kura za kutosha katika raundi ya kwanza ya uchaguzi bungeni, kabla ya kushinda kwenye duru ya pili.
"Tunahitaji kukumbuka kuwa AfD huelekea kulenga hali ya kutojiamini na kuibadilisha kuwa mtaji wa kisiasa. Lakini si kila tatizo la kutafuta wingi wa kura au changamoto serikalini ni ushindi kwa AfD,” alisema.
Kwa mujibu wa Holnburger, wanasiasa wanapaswa kupambana na hali hii kwa kuonyesha mfano wa mafanikio ya demokrasia — kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni nchini Kanada na Australia. "Mgawanyiko unaweza pia kusababisha nguvu mpya za busara kuimarika,” aliongeza.
Utafiti kuhusu mgawanyiko wa kijamii
Mtaalamu Adrian Blattner kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani, anaangazia kwa kina masuala ya mgawanyiko wa kijamii na kisiasa nchini Marekani, Brazil na Ujerumani. Kwa mujibu wa hoja yake, hali ya kile kinachoitwa "mgawanyiko wa kihisia" imeongezeka, lakini bado haijafikia kiwango kilichopo Marekani au Brazil.
Blattner na timu yake waliwasilisha utafiti ulioheshimika sana miaka mitatu iliyopita — uliotokana na shindano la mawazo kuhusu njia bora za kupunguza mgawanyiko. Mawazo 25 yalijaribiwa kwa washiriki 32,000, ikiwemo michezo ya mtandaoni.
Ujerumani pia imeshuhudia mpango kama huo kwa mafanikio sawa. Mwaka 2017, tovuti ya habari Zeit Online iliandaa mradi wa "Germany Speaks," uliowaleta watu wenye mitazamo pinzani ya kisiasa katika majadiliano ya moja kwa moja.
Soma pia: Waziri Faeser asema AfD haipaswi kujinufaisha na tukio la Magdeburg
Blattner alichambua mradi huo mwaka 2021 na kubaini kuwa washiriki walikuwa na hisia chanya zaidi kuhusu wale waliokuwa na maoni tofauti baada ya majadiliano hayo. Anaamini kuwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya wapiga kura wa chama cha kijani mijini na wale wa AfD vijijini yanaweza kuleta maridhiano.
"Baadhi ya wapiga kura wa chama cha Kijani na cha Social Democrat pia wanaunga mkono sera kali zaidi kuhusu uhamiaji, na vilevile kuna wafuasi wa sera za ulinzi wa mazingira miongoni mwa wapiga kura wa AfD,” Blattner aliambia DW.
Ni muhimu, anasisitiza, kutowachukulia wapiga kura wa chama kimoja kama kundi moja lisilobadilika: "Hali hiyo huongeza hisia hasi dhidi ya upande mwingine, watu huacha kuwasiliana, dhana potofu huimarika na mgawanyiko huongezeka. Tunapaswa pia kutafuta njia binafsi za kudumisha mawasiliano na watu wenye mitazamo tofauti — hata kama ni vigumu wakati nyingine.”
Mbali na suala la AfD, masuala ya uhamiaji, ulinzi wa mazingira na mafao ya wasio na ajira yanaonekana kuwa vyanzo vikuu vya mgawanyiko mkubwa miongoni mwa makundi mbalimbali nchini Ujerumani.
Hata hivyo, mchambuzi wa kijamii Kiess anasema, "Bado si kama Marekani ambapo mgawanyiko umejikita sana — haijalishi unajadili suala gani, watu wako upande mmoja au mwingine.” Kwa ujumla, Ujerumani haijagawanyika sana kama inavyodhaniwa. "Mgawanyiko unaoonekana ni mkubwa zaidi ya ule halisi.”