Ujerumani yakabiliwa na mdororo wa kiuchumi
15 Mei 2020Ujerumani taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya limeingia kwenye mdororo wa uchumi kutokana na athari za virusi vya corona, imesema idara ya taifa ya Takwimu ya nchi hiyo. Serikali inajaribu kupunguza makali kupitia mipango yake ya uokoaji uchumi na pia janga hilo limechangia kusinyaa kwa uchumi wa mataifa mengine makubwa Ulaya kama Italia na Ufaransa.
Anguko katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi ni la pili kwa ukubwa katika kipindi cha robo mwaka tangu Ujerumani ilipoungana mwaka 1990. Machi ni mwezi ulioshuhudia janga la corona likiipiga Ulaya ambapo Italia ilikuwa ya kwanza na kisha kufuatiwa na nchi nyingine zilizoweka vizuizi vya shughuli za maisha ya kawaida na biashara.
Kwa mujibu wa data zilizokwisha tolewa mataifa 19 yanayotumia sarafu ya euro uchumi wake ulishuka kwa asilimia 3.8 katika robo ya kwanza kutokana na kwamba shughuli nyingi za biashara zilikuwa zimesimama. Taarifa hiyo pia imeonesha kutakuwa na anguko kubwa zaidi Ujerumani katika robo ya pili ya mwaka 2020 kabla ya kuimarika tena kwa hali ya uchumi.
Wakati huo wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imesema majimbo 16 ya nchini humo yanapanga kuanza kuondoa vizuizi vya kuwaweka karantini wasafiri. Wizara hiyo hivi sasa inafanyia kazi mfumo ambao utatumiwa na kila jimbo kufuatia makubaliano katika mazungumzo na ofisi ya kansela Angela Merkel. Taratibu zinazotumika hivi sasa katika majimbo mengi ya Ujerumani ni kwamba wasafiri wanaotoka nchi za jirani katika Umoja wa Ulaya wanalazimika kukaa karantini ya siku 14.
Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya ambako maambukizi ya kirusi cha corona yanaonekana kupungua, yameanza kuondoa vizuizi vya mpakani. Slovenia iliyoanza polepole kuondoa vizuizi vyake imetangaza kwamba maambukizi ya kirusi hicho sasa yamedhibitiwa na kwamba wakaazi wa Umoja wa Ulaya wanaweza kuingia kutokea Austria, Italia na Hungary. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Slovenia Jelko Kacin.
Huko Urusi kiwango cha maambukizi kimefikia watu 260,000 na kuifanya kuwa nchi ya pili kuwa na maambukizi mengi baada ya Marekani. Idadi ya vifo iliongezeka kwa watu 113 usiku wa leo na kufikia 2,418. Mji wa Moscow ambao ni kitovu cha maambukizi ya virusi hivyo nchini Urusi, Ijumaa hii umeanza zoezi kubwa la upimaji wakaazi wake.