1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakamilisha kampeni kwenda Urusi kwa mafanikio

Sekione Kitojo
9 Oktoba 2017

Ujerumani  kutetea  ubingwa  wa  dunia  nchini  Urusi  mwakani , baada  ya  mafanikio  makubwa  katika  michezo ya  kufuzu  kucheza kombe  la  dunia.

Deutschland Joachim Löw in Mainz
Picha: picture alliance/GES/M. Gilliar

Ujerumani  imefanikiwa  kukata  tikiti  yake  kwenda  katika  fainali  za kombe  la  dunia  nchini  Urusi  mwakani, kwa kuweka rekodi  ya kufunga  mabao 43 katika  kipindi  cha  michezo  ya  kifuzu na kuweza  kutetea  ubingwa  wake ilioupata  nchini  Brazil  mwaka 2014. Ujerumani  imekamilisha  kampeni  yake  ya  kufuzu  kucheza katika  fainali  za  mwakani  kwa  ushindi  wa  mabao 5-1  jana Jumapili  dhidi  ya  Azerbaijan , lakini  kocha Joachim Loew anatarajia  changamoto  kubwa  mno  katika  fainali  hizo.

Kocha Joachim Loew wa UjerumaniPicha: picture-alliance

"ni makosa  kuchukulia kampeni  hii  ya  kufuzu  kucheza  katika fainali  kuwa  kama  kipimo cha  ubora wa timu.  Bila  shaka  kilikuwa kizuri , ilikuwa  ni  mafanikio  ya  wazi," Loew  alisema  kwa  kuvunja rekodi  ya  Uhispania  ya  kufuzu  kucheza  katika  fainali zilizofanyika  nchini Afrika  kusini  mwaka  2010 kwa  tifauti  ya magoli. Lakini  aliongeza  kwamba  "Ngazi  nyingine  inatusubiri katika  kombe  la  dunia.

"Hii  ndio  sababu  tunahitaji  kutuliza  boli chini, bado  kuna  mengi ya  kufanya. Nataka  kufanikisha  kitu  fulani  kwa  maana  sana katika  muda  wa  miezi  michache ijayo. Itakuwa  vigumu kuwa bingwa  wa  dunia  mara  mbili  mfululizo , Loew  alisema  katika mkutano  na  waandishi  habari.

Kwa  upande  mwingine  mshambuliaji  wa  Bayern Munich Robert Lewandowski  aliifungia  timu  yake mabao  ambayo  ni  rekodi katika  michezo  ya  kufuzu  kucheza  katika  fainali  za  kombe  la dunia  wakati  Poland  ikiishinda  Montenegro kwa  mabao 4-2  na kufikia  fainali  hizo  nchini  Urusi  mwakani. Lewandowski  alifunga mabao 16  katika  kampeni  ya  Poland  kuelekea  Urusi  mwakani. Poland  imefanikiwa  kufunga  safari  kwenda  katika  fainali  ya kombe  la  dunia  kwa  mara  ya  kwanza  tangu  mwaka  2006.

Mshambuliaji wa Poland Robert LewandowskiPicha: picture-alliance/ZUMA Press/NurPhoto/Foto Olimpik

England haina nafasi

England imekata  tikiti  yake  katika  fainali  za  kombe  la  dunia , lakini  nafasi  yake  kuweza  kuonesha  ubavu  wake  nchini  Urusi  ni ndogo kutokana  na  historia  yake  ya  hivi  karibuni. Kikosi  cha kocha  Gareth Southgate kilikamilisha  kampeni  yake  ya  mafanikio katika  kundi  F kwa  ushindi  wa  bao 1-0  nchini  Lithuania  jana Jumapili, na  kurefusha  rekodi  yake  ya  kutofungwa  katika michezo  hiyo  kufikia  michezo  39.

Southgate  hata  hivyo atakuwa na  matumaini  madogo  kutokana  na  kampeni  hiyo , wakati England mara  kadhaa imefanikiwa  kufuzu  katika  michuano  ya kufuzu , na  kisha  kulazimika  kutolewa  katika  fainali  katika  wakati ambapo  timu  hiyo  inamatumaini  makubwa  ya  kusonga  mbele katika  fainali  za  kombe  la  dunia.

Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Gareth SouthgatePicha: Imago/Eibner Europa

Katika  historia  ya  miaka  51 tangu  pale  Uingereza  iliposhinda kwa  mara  ya  kwanza  kombe  la  dunia  katika  ardhi  yake, hadhi ya  timu  hiyo  ya  taifa  imechafuliwa  kwa  kiasi  kikubwa  ambapo mashabiki waligeuka  na  kuipa   mgongo wakati ilipofanikiwa  kukata tikiti  yake  dhidi  ya  Slovenia siku  ya  Alhamis.

Wakati  uwanja  wa  Wembley ukiwa  umejaa  nusu , England ilishuhudia  mashabiki  wakiwa  hawana  hamu  tena kutokana  na mchezo uliopooza na  usio  na  mbinu na  msisimko  na  kurusha mfano  wa  ndege  ya  karatasi uwanjani  na  kushangiria watu waliovamia  uwanja.

Wachezaji nyota

Makocha wa zamani  wa  England waliweza  kutumia  kikosi chenye nyota wengi  kuliko kikosi  cha  sasa  cha  Southgate , lakini  kuwaita kikosini  wachezaji  wa  nyumbani  hakuna  uhakika  wa  mafanikio. katika  enzi  za  Sven Goran Eriksson , wachezaji  kama  Steven Gerrard , Frank Lampard, John Terry, Paul Scholes, David beckham na  wayne  Rooney  walikuwa  wote  miongoni  mwa  wachezaji  bora kabisa  kwa  vilabu  vyao, wakiwa  wamepata  mataji  pamoja  na mafanikio  katika  Champions League.

Mchanganyiko wa wachezaji wa zamani na wa sasa wa EnglandPicha: picture-alliance/Sven Simon/F. Hoermann

Southgate  ana  kikosi  ambacho  hakina  majina  makubwa  sana  na uzoefu  mkubwa , na  hata   nyota  wake wakubwa  Harry Kane  na Dele Ali  bado  hawajapata  tuzo  kubwa  katika  vilabu  vyao  na Marcus Rashford  ndio  kwanza  anaanza  kuonesha uwezo  wake.

Harry Kane mshambuliaji wa UingerezaPicha: Reuters/D. Staples

Michezo  ya  kufuzu  kucheza  katika  fainali  za  mwakani  za  kombe la  dunia  inaendelea  tena  leo  ambapo  Moldavia  itakwaana  na Austria , Wales  ina  miadi  na  Ireland, Albania  itawakaribisha Wataliani mjini  mwao  na  Ukraine  itaoneshana  kazi  na  Croatia.

Uhispania  inakwaana  na  Israel  huku  mzozo  wa  kujitenga  kwa jimbo  la  Catalonia  ukiendelea. Hali  ya  hatari  hata  hivyo inaikabili  Uholanzi.  Kikosi  hicho  cha  Wadachi  kinakabiliana  na Sweden kesho ambapo timu  hizo  zinatengana  kwa  pointi  tatu.

Nahodha wa Uhispania Gerard PiquePicha: picture-alliance/AP Photo/G.Ehrenzeller

Sweden  ina  pointi 19 , wakati  Wadachi Uholanzi  ina  pointi  16 , na  tofauti  kubwa  pia  ya  magoli. Uholanzi  inahitaji  kushinda mchezo  huo  na  kupata  zaidi  ya  mabao 7 kitu  ambacho ni kigumu. Kocha  wa  Sweden  Janne Andersson  amesema.

"Ni mchezo  maalum sana,  na  tunahisi  kwamba  Wadachi watacheza  mchezo  wa  kushambulia  mno, lakini tumekwisha  cheza michezo  kama  hiyo  hapo  nyuma  dhidi  ya  timu  kama  hizo, na Sweden itapanga  mchezo  wake  kama  inavyofikiria kwamba  ni sahihi  kwa  hali  hiyo."

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / ape / afpe / dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW