1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakataa maelezo ya Urusi kuhusu Nord Stream 1

18 Julai 2022

Wakati athari za vita nchini Ukraine zikianza kuzielemea chumi za Ulaya, Ujerumani imeyakanusha madai ya Urusi kwamba kuna matatizo ya kiufundi yaliyoifanya kupunguza kiwango cha gesi kupitia bomba la Nord Stream 1.

Russland | Portovaya Kompressionsstation
Picha: Nord Stream Ag/ZUMA Wire/IMAGO

Serikali ya Ujerumani imesema hivi leo kwamba kinu ambacho kimekuwa kiini cha utata juu ya mustakabali wa bomba la kufikisha gesi ya Urusi barani Ulaya kilitakiwa kiwe kimeshajengwa kufikia mwezi Septemba mwaka huu, na kwa hivyo hakuna ukweli wowote kwamba kuna kikwazo cha kuifikisha gesi hiyo kwa sasa.

Kauli ya Ujerumani baada ya kampuni ya uuzaji gesi ya Urusi, Gazprom, kupunguza usafirishaji wa gesi kupitia bomba la Nord Stream 1 kwa asilimia 60 kuelekea Ujerumani mwezi uliopita, ikidai kwamba kuna matatizo ya kiufundi, baada ya mshirika wake Siemens Energy kutuma vifaa kwa ajili ya mabadilishano nchini Canada, na ambacho kimeshindwa kurejeshwa kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

Wanasiasa nchini Ujerumani wameyakataa maelezo ya kiufundi yaliyotolewa na Urusi, wakisema kuwa ni uamuzi wa kisiasa uliochukuliwa na Kremlin ili kupandikiza hali ya wasiwasi na kupandisha bei ya nishati hiyo.

"Hatuoni sababu yoyote ya kiufundi. Taarifa tulizonazo ni kwamba mtambo huo ni wa kuchukuwa nafasi ya mwengine ambao ulikuwa uwekwe mwezi Septemba, lakini tunajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuondosha visingizio vya Urusi." Msemaji wa wizara ya uchumi ya Ujeruamni, Beate Baron, aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Jumatatu (Julai 18).

Utata wa gesi ya Urusi

Bomba kuu la Nord Stream 1 Picha: Stefan Sauer/dpa/picture alliance

Wiki iliyopita, serikali ya Canada ilisema ingeliruhsuu kufikishwa kwa mtambo huo nchini Ujerumani, ikirejelea wasiwasi wake juu ya hali ngumu itakayoukumba uchumi wa Ujerumani endapo haitakuwa na gesi ya kutosha kuendeshea viwanda vyake. 

Bomba laNord Stream 1 lilifungwa kwa matengenezo ya mwaka tarehe 11 mwezi huu wa Julai, na maafisa nchini Ujerumani wana wasiwasi kwamba Urusi inaweza isirejeshe usafirishaji gesi baada ya kazi ya matengenezo kumalizika Alkhamis wiki hii. 

Hayo yanajiri wakati Rais Vladimir Putin anatazamiwa kuzungumza na mwenzake wa Uturuki, Tayyip Erdogan, siku ya Jumanne (Julai 19) juu ya usafirishaji wa ngano kutoka Ukraine.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema kwamba viongozi hao wawili watakutana mjini Tehran, Iran, ambako pia wataungana mwenyeji wao, Ibrahim Raees, kwenye mazungumzo yatakayojadili pia suala la vita nchini Syria.

Wawakilishi wa Urusi, Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kusaini makubaliano juu ya suala hilo baadaye wiki hii, wakidhamiria kurejesha usafirishaji wa ngano na bidhaa nyengine za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi, ambayo imetwaliwa na Urusi tangu uvamizi wake dhidi ya Ukraine ulioanza mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW