Ujerumani yakiri kitisho cha itikadi kali
21 Februari 2020Seehofer amewaambia waandishi wa habari hii leo mjini Berlin kwamba kutokana na shambulizi hilo, kutaimarishwa hatua za ulinzi wa polisi kote nchini Ujerumani ili kukabiliana na kitisho cha juu cha kiusalama kutoka kwa wafuasi hao wa siasa kali za mrengo wa kulia, ambacho amekiri kumefikia kiwango cha juu mno.
Seehofer alisema "tutahakikisha polisi wanakuwepo kwa wingi katika sehemu zote nchini Ujerumani. Tutaongeza ulinzi hasa kwenye maeneo nyeti kama kwenye misikiti. tutaongeza ulinzi kwenye vituo vya treni, viwanja vya ndege na maeneo yaliyo karibu na mipakani."
Ujerumani, tayari imekwishachukua hatua kadhaa za kupambana na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia baada ya msururu wa visa vya mashambulizi mwaka uliopita wa 2019. Seehofer amesema, hatatoa mwito wa kuongezwa idadi ya polisi ama sheria nyingine mpya ya kupambana na kitisho hicho, na badala yake wataendelea kutumia kwa ukamilifu machaguo ambayo tayari yapo.
Waziri wa sheria wa Ujerumani Christine Lambercht amesema serikali itachunguza kwa kina namna ambavyo silaha huishia mikononi mwa watu wenye itikadi kali. Hata hivyo kwa pamoja mawaziri hao wamekiri ugumu katika kuwabaini washambuliaji wanaofanya mashambulizi peke yao, kuwa ndio wahusika muhimu kwenye shambulizi hilo la Hanau.
Mkuu wa jeshi la polisi Holger Muench kwa upande wake ameonya kwamba takriban nusu ya wale wanaofanya mashambulizi kama hayo hawakutambuliwa na mamlaka huko nyuma.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, AfD kinachonyooshewa kidole kufuatia sera zake za chuki dhidi ya wageni hii leo kimeungana na vyama vingine vya siasa kufuta mkutano wa kampeni za mwisho za ajili ya uchaguzi kwenye jiji la Hamburg, kaskazini mwa Ujerumani kufuatia shambulizi hilo. Uchaguzi huo unafanyika Jumapili hii.
Maafisa wa chama hicho wamesema hawakutaka tawi lao la Hamburg kushutumiwa kwa kukosa nidhamu.
Chama cha Social Democrats, SPD kinachounda serikali ya muungano na CDU, kimetaka AfD ambacho ni mpinzani mkubwa bungeni kufuatiliwa. Lakini, kiongozi wa chama hicho kwenye bunge hilo Alexander Gauland amepuuzia miito hiyo akisema kutaka kuutumia uhalifu uliofanywa Hanau dhidi yao ni jambo baya sana.
Mwanasiasa mwenye umaarufu wa chama cha Kijani Cem Ozdemir amekielezea chama hicho cha AfD kama tawi la kisiasa la chuki, wakati akizungumza na kituo cha radio cha umma cha Ujerumani.
Sheria za Ujerumani zinaruhusu uchunguzi kufanywa na mashirika ya kijasusi pale yanapohisi kuna ishara za misimamo mikali.
Katika hatua nyingine, serikali ya Ujerumani hivi sasa inakabiliwa na miito ya kuimarisha sheria za umiliki wa silaha na kuchukua hatua zaidi za kuwafuatilia wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia baada ya mtuhumiwa wa mashambulizi mabaya kabisa ya mauaji tangu vita yva pili vya dunia kukutwa kiwa amechapisha ilani yenye maudhui ya ubaguzi wa rangi.