1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakosolewa kuhusu misaada ya maendeleo

9 Novemba 2010

Dirk Niebel alipinga vikali misaada ya maendeleo alipokuwa upande wa upinzani na aliitaka wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ijumuishwe na wizara ya mambo ya nje.

German Minister for Economic Cooperation and Development, Dirk Niebel listening at speech the environmental education project started between Germany, Brazil and Peru, in Lima, 02 November 2010. Photo: Marco Garro/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani,Dirk Niebel.Picha: dpa

Sasa yeye ni waziri wa maendeleo na hataki kuivunjawizara hiyo bali anataka mageuzi kadhaa - yaani maslahi ya Ujerumani yazingatiwe zaidi.Mwaka mmoja umeshapita, tangu Niebel kushika madaraka yake mapya,kwa hivyo, mashirika mawili ya misaada ya Ujerumani, yamechunguza yale yaliyofikiwa. Ujerumani imeahidi kutoa angalao asilimia 0 .7 ya pato lake la jumla la ndani kwa misaada ya maendeleo ifikapo mwaka 2015. Lakini kwa mujibu wa mashirika mawili ya misaada ya Ujerumani, "Welthungerhilfe" na "Terre des Hommes" msaada uliotolewa ni asilimia 0.35 tu ya pato la jumla la ndani.Msaada huo unapaswa kuongezeka hadi asilimia 0.7 ifikapo mwaka 2015. Katibu Mkuu Wolfgang Jamann wa "Welthungerhilfe" anasikitika kuwa hilo wala si jipya, kwani hutokea mara kwa mara. Anasema:

"Kila mwaka tunashindwa kufikia malengo yaliyokubaliwa na yanayopaswa kutekelezwa.Kwa kweli,kunahitajiwa Euro bilioni mbili za ziada kila mwaka, ili kuweza kufikia lengo hilo katika mwaka 2015."

Hiyo humaanisha bajeti ya mwaka huu wa 2010 iongezwe kwa Euro milioni 256 - lakini baadae hakutokuwepo ongezeko jingine. Wakati ambapo baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kama vile Uholanzi,Sweden au Denmark zimefikia kiwango cha asilimia 0.7 kilichowekwa, wanachama wengine wamejitahidi kuongeza msaada wao wa maendeleo. Jamann amelinganisha bajeti ya misaada ya maendeleo iliyoongezwa na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya kati ya mwaka 2008 na 2009.

Danuta Sacher wa Terre des Hommes(kulia) na Wolfgang Jamann wa Welthungerhilfe.Picha: Welthungerhilfe

Mashirika hayo mawili kila mwaka hutathmini misaada ya maendeleo inayotolewa na serikali ya Ujerumani na hutoa ripoti ya pamoja inayoitwa "Ukweli wa misaada ya maendeleo". Na mwaka huu ripoti hiyo imekosoa vikali. Serikali ya muungano wa vyama ndugu vya kihafidhina CDU na CSU na chama cha kiliberali cha FDP, ipo madarakani tangu mwaka 2009. Na waziri wa maendeleo Dirk Niebel wa FDP hakuwa tu maarufu kama mkosoaji mkali wa wizara ya ushirikiano wa kiuchumi, kwani baada ya kushika madaraka, alitangaza kuwa misaada ya maendeleo itazingatiwa kuambatana na maslahi ya kiuchumi ya Ujerumani. Danuta Sacher wa shirika la "Terre des Hommes" anasema:

"Tatizo ni kwamba shughuli za kiuchumi zinaelekezwa kule ambako mauzo na faida ni ya juu. Na hali hiyo haiwezi kulinganishwa na zile nchi na sekta pamoja na jamii ya wakaazi waliotengwa na wanaohitaji sana misaada ya maendeleo."

Kwa mfano mwaka 2009, Ujerumani iliitaka Mexico kutumia makampuni ya Kijerumani katika ujenzi wa bandari yake na Namibia kwenye kiwanda cha saruji. Hata hivyo, ripoti hiyo haipuuzi miradi yote lakini inasema vigezo vya kutoa msaada wa fedha si wazi. Miradi mingi hujadiliwa kati ya makampuni na wizara bila ya mwishowe kutangaza matokeo yaliyofanyiwa uchunguzi.

Mwandishi:Bölinger,Matthias/ZPR

Mpitiaji: Charo,Josephat