Ujerumani yaleta raha nyumbani
6 Julai 2011Ujerumani jana iliweza kumaliza mchezo wake wa kundi A, kwa kuongoza baada ya kuicharaza Ufaransa mabao manne kwa mawili, huku moja ya mabao hayo likipatikana kwa njia ya adhabu waliyopewa Ufaransa, iliyosababisha pia golikipa wao Berangere Sapowicz, kupewa kadi nyekundu, baada ya kumvamia mchezaji wa Ujerumani Fatmire Bajramaj katika eneo la hatari.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo Ujerumani iliweza kujiweka vizuri katika nafasi ya ushindi, baada ya kupata mabao mawili yaliyofungwa na Kerstin Garefrekes na Inka Grings, ambaye ndiye pia aliyefunga bao la tatu lililopatikana kwa njia ya adhabu, katika kipindi cha pili.
Celia Okoyino da Mbabi alilizamisha kabisa jahazi la Ufaransa baada ya kupachika goli la nne, lililowaongezea furaha Wajerumani.
Akizungumzia mchezo huo Inka Grings wa Ujerumani, ambaye alitoka kifua mbele katika mchezo huo wa jana baada ya kupachika magoli mawili alisema walicheza vizuri sana.
Amesema pia ushindi huo ni muhimu kwa timu yao. na kwamba waliumiliki mchezo na mashabiki wao wameona kwamba wamemecheza mchezo mzuri sana. na kuweza kuichezea vizuri timu yao.
Kwa upande wake kocha wa Ujerumani, Silvia Neid, pia alisifia mchezo huo.
Amesema ilikuwa mechi nzuri . Tangu mwanzo hawakupoteza kila fursa waliyoipata. Pasi zao zilikuwa safi, kasi yao kwenda mbele ilikuwa nzuri. Kwake yeye anasema ulikuwa ni mpira wa miguu hasa.
Magoli mawili ya Ufaransa yalifungwa na Marie-Laure Delie na Laura Georges.
Na katika mchezo mwingine wa kundi A, uliochezwa jana, wawakilishi wa Afrika ambao tayari wameshafungishwa virago, Nigeria, hawakutaka kuondoka watupu, baada ya kuikung'uta Canada bao moja kwa bila. Huku Uingereza nayo ikifanikiwa kuongoza kundi B, baada ya kuichabanga Japan mabao mawili kwa bila. New Zealand nayo ikitoka sare ya kufungana mabao wawili kwa wawili na Mexico.
Michuano hiyo ya kombe la dunia la soka la wanawake mwaka 2011, inaendelea tena leo, kwa timu nane kujitupa uwanjani. wawakilishi wengine wa Afrika Guinea ya Ikweta watapambana na Brazil, huku Australia wakivaana na Norway.
Sweden itakutana na Marekani. Korea kaskazini nayo itacheza na Colombia.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp, dpa, Reuters)