1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Ujerumani yalia na njama ya kumuua mkuu wa kampuni ya silaha

12 Julai 2024

Wanasiasa wa Ujerumani wameeleza kughadhabishwa na ripoti kwamba Urusi ilipanga kumuua mkuu wa kampuni ya kutengeneza silaha ya Ujerumani ya Rheinmetall, Armin Papperger. Urusi imepuuza taarifa hizo na kuziita uongo.

Ujerumani | Armin Papperger akiwa mkutano wa ufufuaji wa uchumi wa Ukraine
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya silaha ya Rhein Metall, Armin Papperger, ambaye amekosoa waziwazi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, alipewa ulinzi maalum.Picha: Thomas Trutschel/photothek.de/AA/picture alliance

Kikinukuu maafisa wa Marekani na magharibi ambao haikuwataja majina, kituo cha televisheni cha CNN kiliripoti kuwa Marekani iliiarifu Ujerumani kuwa serikali ya Urusi ilikuwa na mpango wa kumuuwa Armin Papperger, mkuu wa kampuni ya silaha ya Rheinmetall.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alikataa kutoa ufafanuzi kuhusu ripoti hiyo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington.

"Hii ndiyo hali ya kila siku. Wakati huo huo ninafurahi kukuambia kwamba tunajua vyema kuwa tunakabiliwa na vitisho mbalimbali kutokana na shughuli za Urusi na kwamba tunazifuatilia kwa umakini mkubwa," alisema Scholz mjini Washington.

Wanasiasa wa Ujerumani wameeleza kushtushwa na ripoti hiyo, huku mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya Bunge la Ujerumani - Bundestag, Marcus Faber, akisema njama hiyo inaonyesha kuwa Urusi pia inaleta vita vyake na ugaidi barani Ulaya, na kuongeza kuwa utawala wa Putin unatafuta pia maisha ya raia wa Ujerumani.

Markus Faber, kulia, amesema Urusi inahamisha vita vyake na ugaidi barani Ulaya.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma pia: Jeshi la Ujerumani lina utayari kubeba dhamana NATO?

Naye mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya Bundestag, Michael Roth, alisema katika mahojiano na gazeti la Bild kuwa Rais wa Urusi Vladmir Putin siyo tu anaendesha vita vya kuiangamiza Ukraine, lakini pia dhidi ya wanaoiunga mkono na maadili yao.

Mtaalamu wa sera ya ulinzi wa chama cha upinzani cha Christian Democratic Union, CDU, Serap Güler, alisema majibu ya Ujerumani kwa njama hiyo yanapaswa kuwa kuongeza msaada kwa ajili ya Ukraine.

Kando ya mkutano wa kilele wa NATO, Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock alisema Urusi inaendesha vita mseto vya uchokozi katika nchi za Magharibi, bila kutaja njama yoyote kwa uwazi, na kuongeza kuwa watu binafsi na makampuni yalishambuliwa.

Kremlin yasema ni upuuzi mtupu!

Ikulu ya Kremlin imepuuza ripoti hiyo ambayo ambapo msemaji wake Dmitry Peskov amesema ni vigumu kuzungumzia ripoti za vyombo mbalimbali vya habari zisizo na hoja zozote nzito na zinazotegemea vyanzo visivyotajwa.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema ripoti za njama ya kumuua Papperger ni upuuzi na zisizo na ukweli.Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa jarida la kila wiki la Spiegel, mashirika ya ujasusi ya magharibi yaliwatambua washukiwa kadhaa wanaohusishwa na njama dhidi ya Papperger, wakitokea mataifa yaliokuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti, akiwemo alau raia moja wa Urusi.

Soma pia: Zelensky ahimiza Ukraine isigawanywe na Urusi

Idara za usalama ziliamini washukiwa hao walikuwa mawakala wa idara ya ujasusi ya Urusi, lakini ushahidi dhidi yao ulikuwa hautoshi ili kuweza kuwakamata, kulingana na jarida la Spiegel.

Baada ya maafisa wa Ujerumani kuarifiwa kuhusu mpango huo, mkuu huyo wa kampuni ya silaha mwenye umri wa miaka 61 - ambaye amekosoa waziwazi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine - alipewa ulinzi maalum.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW