1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaondowa vikwazo vya safari kwa COVID-19

1 Oktoba 2020

Hatimaye Ujerumani imeondosha marufuku yake ya safari kwa nchi zote ambazo hazipo kwenye Umoja wa Ulaya, huku kila dalili zikionesha kuwa wimbi jipya la maambukizo ya virusi vya corona linaanza tena barani Ulaya.

Deutschland Berlin | Beratungen über die Corona-Pandemie
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Kufunguliwa huko upya kwa mipaka na viwanja vya ndege kuliamuliwa na baraza la mawaziri wiki tatu zilizopita, lakini utekelezaji wake umeanza Alkhamis ya leo. Mataifa 160 duniani yanafaidika na uamuzi huu.

Hata hivyo, uamuzi huu unaanza kutekelezwa wakati idadi ya maambukizo mapya ya COVID-19 ikipanda barani Ulaya, huku wengi wakionya kwamba bara hili limo kwenye ukingo wa kutumbukia kwenye awamu ya pili ya janga la virusi vya corona. 

Ujerumani ilitowa indhari ya safari kwa ulimwengu mzima mnamo mwezi Machi, wakati virusi hivyo vikisambaa kwa kasi kaskazini mwa Italia, lakini ikaiondosha kwa mataifa mengi ya Ulaya mwezi Juni. 

Mwezi uliopita, Ujerumani ilianza tena kutangaza tahadhari kwa maeneo kadhaa ya Ulaya, baada ya maambukizo kuanza tena kupanda kwa watu 50 katika kila 100,000 kwa wiki.

Taasisi ya Robert Koch inayoshughulika na udhibiti wa maradhi nchini Ujerumani imeyatangaza maeneo 11 barani Ulaya ambayo yana kiwango kikubwa cha maambukizo ya virusi vya corona, zikiwemo Ubelgiji, Iceland, Wales na Ireland ya Kaskazini.

Maambukizo yaanza tena kupanda

Kansela Angela Merkel ametaka hatua kali ziendelee kuchukuliwa kudhibiti wimbi jipya la virusi vya corona.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Idadi ya maambukizo imepanda nchini Ujerumani kwa wagonjwa wapya 2,503 hivi leo na hivyo kufikisha watu 291,722 waliokwishaambukizwa virusi vya corona, huku wengine 12 wakipoteza maisha.

Hadi sasa Ujerumani imeshapoteza watu 9,500 kutokana na janga hilo la kilimwengu.

Utaratibu huu utatumika pia kwenye siku zijazo, ambapo wale wanaotokea kwenye maeneo ambayo idadi ya maambukizo ni ya chini wataruhusiwa kuingia Ujerumani bila kulazimika kukaa karantini. Kwa sasa, kuingia na kutoka Ujerumani bila vikwazo vyovyote kutakuwa ni kwa baadhi ya maeneo tu ya Ulaya na Georgia. 

Mabadiliko haya yanaweza kuwa na umuhimu kwa maeneo ya kitalii nje ya Ulaya ambayo kawaida huwa yanapokea wageni wengi kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya yenye wakaazi wengi.

Safari kuelekea nchini Uturuki, ambayo ni chimbuko la takribani raia wake milioni nne wa Ujerumani, zimeruhusiwa kwa masharti maalum, ambapo wale wanaolekea miji kadhaa ya pwani ya nchi hiyo wamekubaliwa ikiwa tu kwanza watapima virusi vya corona kabla ya kurejea Ujerumani.

Chini ya kanuni hizo mpya, wizara ya mambo ya kigeni imepewa mamlaka ya kuendelea kutoa maonyo dhidi ya kusafiri kwenda nchi ambazo zimewekwa vikwazo dhidi ya watu wanaowasili kutokea Ujerumani, zikiwemo Australia, China, Canada, Rwanda na Uruguay.