1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaongeza muda wa marufuku kwa safari za kitalii

29 Aprili 2020

Katika juhudi za kupambana na janga la Corona Ujerumani imeongeza muda wa kupiga marufuku safari za kitalii hadi katikati ya mwaka huu. Kwingineko barani Ulaya hatua za kuwazuia watu majumbani zimeendelea kulegezwa.

Deutschland Franz-Josef-Strauss Flughafen München Bayern Flugzeuge Lufthansa
Picha: Getty Images/C. Stache

Baraza la mawaziri la Ujerumani limepitisha uamuzi wa kuongeza muda wa kupiga marufuku safari za kitalii katika nchi za nje, hadi mwezi wa Juni. Waziri wa mambo ya nje Heiko Maas anaeleza juu ya uamuzi huo:

"Tulilazimika kuchukua uamuzi huo kwani kwa sasa hatuko tayari kuwashauri watu wasafiri nje wapendavyo, wakati ambapo tunapambana na maambukizi ya virusi vya corona. Bado nchi nyingi zimeweka vizuizi katika kuingia na kutoka na usafiri wa anga duniani umesimama.” 

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema Ujerumani itaendelea kujadiliana na washirika wake wa Ulaya juu ya suala hilo.

Zaidi ya 160,000 wameambukizwa virusi vya corona na zaidi ya 6000 wamekufa Ujerumani. Wakati huo huo uchumi wa Ujerumani unatarajiwa kunywea kwa zaidi ya asilimia 6 mnamo mwaka huu kutokana na athari za maambukizi ya virusi vya corona.

Nchini Urusi, waziri mkuu wa nchi hiyo Mikhail Mishustin ameeleza kuwa nchi yake pia imeongeza muda wa kupiga marufuku watu kutoka nje kuingia nchini Urusi.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: Getty Images/F. Singer

Watu takriban 100,000 wameambukizwa nchini humo na 972 wameaga dunia.

Kwingineko barani Ulaya nchi kadhaa zimeanza kulegeza hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya corona hata hivyo tahadhari zimetolewa.

Nchini Marekani idadi ya watu waliioambukizwa virusi vya corona imeshavuka milioni moja na waliokufa ni zaidi ya 58,000.

Wakati huo huo rais Donald Trump amekanusha madai kwamba utawala wake ulichelewa kuchukua hatua za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, badala yake Trump amesisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa na utawala wake zimeokoa maisha ya wamarekani wengi.

China imebadilisha tarehe ya mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti uliokuwa ufanyike tarehe 22 mwezi Mei na Uturuki imeongeza muda wa kufunga shule hadi mwishoni mwa mwezi ujao.

Na Singapore imezindua matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani kupeleka mahitaji ya dawa na hivyo kuepusha maambukizi.

Vyanzo:/AFP/AP/DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW