1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapiga marufuku mikusanyiko hadi mwisho wa Oktoba

17 Juni 2020

Kansela Angela Merkel amekubaliana na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya Ujerumani kupiga marufuku mikusanyiko yote mikubwa hadi mwishoni mwa mwezi Oktoba katika jitihada za kulikabili janga la virusi vya korona.

Deutschland Berlin Pressekonferenz zum Konjunkturpaket | Angela Merkel
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Mkutano huu wa Jumatano (Juni 17) ulikuwa wa kwanza wa ana kwa ana kati ya Kansela Merkel na mawaziri hao wakuu wa majimbo, baada ya miezi mitatu ya kuzungumza nao kwa njia ya vidio na simu.

Mkutano wa mwisho wa ana kwa ana baina yao ulikuwa ni tarehe 12 Machi, ambao ndio uliotoka na maazimio ya kuifunga  moja kwa moja nchi na kusababisha shughuli zote za maisha kusimama.

Kwa mujibu wa waraka kuhusu sera uliopatikana na mashirika ya habari, matamasha na mikusanyiko yote mikubwa inaendelea kupigwa marufuku hadi angalau mwishoni mwa mwezi Oktoba kwa khofu kwamba virusi vya korona vitasambaa upya. 

Lakini kwenye upande wa masomo, serikali kuu ilikuwa inataka wanafunzi warejee shule baada ya mapumziko ya kiangazi kumalizika, ingawa inapendekeza utaratibu wa kuweka masafa kati ya mtu na mtu na uvaaji barakowa uendelezwe kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko, kama vile madukani na usafiri wa umma.

Miongoni mwa matukio makubwa na muhimu yatakayoathirika na uamuzi huu ni Tamasha la Kimataifa la Vitabu la Frankfurt. Awali, waandaaji wa tamasha hilo, ambalo hutembelewa na watu zaidi ya 300,000 kila mwaka, walikuwa wamesema hadi sasa wanaendelea na matayarisho kama kawaida. 

Baada ya kushuhudia idadi ya maambukizo ikishuka mwezi Machi na idadi ndogo kabisa ya vifo kulinganisha na majirani zake, Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kuanza kulegeza masharti ya kukabiliana na mripuko wa korona kiasi wiki sita zilizopita. 

Waziri Mkuu wa Bavaria, Markus Soeder (kushoto) na Waziri wa Afya wa Serikali Kuu Jens Spahn kabla ya mkutano wao na Kansela Merkel mjini Berlin tarehe 17 Juni 2020.Picha: picture-alliance/AP/M. Schreiber

Hata hivyo, serikali ya Ujerumai imesema inatambuwa kwamba kudumisha kanuni za kuweka masafa ya mita moja unusu kati ya mtu na mtu na pia kuvaa barakowa kwenye maeneo ya umma kumesaidia sana kwenye vita dhidi ya COVID-19.

Khofu ya maambukizo mapya

Kwa sasa, serikali hiyo imeelekeza nguvu kubwa kwenye kufuatilia watu waliokutana na waliokwishaambukizwa ili kuhakikisha kuwa wenye maambukizo wanawekwa sehemu maalum za uangalizi.

Vile vile, serikali imeazimia kufanya vipimo vya makundi makubwa ya watu, hasa kwenye maeneo ambayo yako kwenye hatari kubwa zaidi ya maambukizo.

Mwenyewe Kansela Merkel anaonekana kutokuwa na haraka hata kidogo ya kuufunguwa tena kikamilifu uchumi na shughuli za maisha, akionya kwamba huko kutakuwa kurejesha nyuma mafanikio yaliyokuwa yamepatikana kwenye vita hivi, hasa katika wakati ambapo hakujawa na chanjo. 

Miongoni mwa matukio yaliyorejesha upya khofu ya kusambaa kwa korona, ni wafanyakazi 400 wa machinjio ya wanyama ya Rheda-Wiedenbruck, magharibi mwa Ujerumani, waliokutwa na virusi vya korona. Nako kwenye mji mkuu, Berlin, familia 370 zimewekwa kwenye karantini baada ya watu 70 kwenye jengo moja kukutwa wameambukizwa virusi hivyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW