1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapinga hatua za kijeshi dhidi ya Libya

Abdu Said Mtullya16 Machi 2011

Ujerumani imepinga kwa mara nyingine matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya utawala wa Gaddafi

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.Picha: dapd

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kwa mara nyingine amepinga wazo la kuifunga anga ya Libya ili kuzizuia ndege za Gaddafi kuruka.

Waziri Westerwelle ameyasema hayo mjini Berlin katika tamko rasmi la serikali ya Ujerumani juu ya hali ya kisiasa nchini Libya.Waziri huyo ameusisitiza msimamo huo licha ya majeshi ya Gaddafi kusonga mbele kuelekea kwenye ngome ya waasi.

Westerwelle ameeleza kuwa Ujerumani haipaswi kuwa pande mojawapo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.Amesema Ujerumani haitaki na wala haipaswi kuwa vitani nchini Libya.Ameeleza kuwa kuchukua hatua za kijeshi ili kuifunga anga ya Libya kutaleta maswali mengi zaidi kuliko majibu.

Akifafanua msimamo wa Ujerumani juu ya nchi za Kaskazini mwa Afrika kwa jumla Waziri Westerwelle alitamka kuwa Ujerumani inataka kusaidia ili watu waweze kuona mustakabal mzuri katika nchi zao. Amesema kuchukua hatua sasa katika nchi hizo ndiyo siasa bora, ili pia kuepusha wimbi la wakimbizi.

Hata hivyo Waziri Westerwelle amesisitiza katika tamko la serikali mjini Berlin leo kwamba badala ya hatua za kijeshi, vikwazo vinapaswa kulengwa panapostahili dhidi ya utawala wa Gaddafi. Kwa hiyo amesema Ujerumani inaunga mkono hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuimarisha shinikizo la kisiasa dhidi ya utawala wa Kanali Gaddafi.

Waziri huyo pia ameyapinga manufaa ya kiuchumi yaliyodokezwa na utawala wa Gaddafi kwa Ujerumani. Waziri Westerwelle ametamka wazi kwamba dikteta Gaddafi lazima aondoke. Amesema urafiki wenye sumu wa dikteta Gaddafi hautaubadili msimamo huo wa Ujerumani.Hapo awali Kanali Gaddafi aliusifu msimamo wa Ujerumani juu ya utawala wake, kulinganisha na ule wa nchi nyingine.

Gaddafi alisema katika mahojiano na televisheni ya RTL kwamba sasa hana imani tena na nchi za magharibi. Na kutokana na hayo tenda za biashara ya mafuta zitakwenda Urusi, China na India. Gaddafi pia amesema anaamini kuwa Ujerumani pia inaweza kuendelea kupata tenda ya biashara ya mafuta.

Juu ya harakati za kuleta mapinduzi ya kidemokrasia katika nchi za Kaskazini mwa Afrika, Waziri Westerwelle amesema Ujerumani pia inashuhudia mapambazuko ambayo ni fursa kubwa kwa nchi hizo na kwa Ujerumani kadhalika.

Waziri huyo pia amezungumzia juu ya hali ya mvutano nchini Bahrain. Ametoa mwito kwa nchi za eneo la Uarabuni wa kujizuia, na amezitaka pande za serikali na za upinzani zianzishe mazungumzo.Amesema suluhisho lazima lipatikane kutokea ndani.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Westerwelle pia ametoa mwito wa kukomesha matumizi ya nguvu.

Mwandishi: Abdul-Mtullya / dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman



Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW