Ujerumani yapinga kuchukua wakimbizi wa Tunisia
16 Februari 2011Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani amepinga katu katu Ujerumani kuwachukua wakimbizi wa Tunisia.
Waziri huyo Thomas de Maiziere amesema kuwa mwaka jana nchi yake iliwapa hifadhi wakimbizi alfu 40 wakati idadi ya wale waliochukuliwa na Italia haikufikia hata alfu saba.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni waziri Thomas de Maiziere alisema kuwa Ujerumani haiwezi kuyatatua matatizo yote ya dunia.Waziri huyo pia ametoa mwito kwa watu wa Tunisia, wa kushiriki katika juhudi za kujenga demokrasia nchini , baada ya Rais Zine El -Abadine Ben- Ali kuangushwa, badala ya kuihama nchi yao.
Wakimbizi zaidi ya alfu tano kutoka Tunisia wameshawasili kwenye kisiwa cha Italia cha Lampedusa tokea, Rais Ben Ali alipoangushwa na kukimbia nchini.Wakimbizi hao wametumia mashua kufika kwenye kisiwa hicho kilichopo katika bahari ya Mediterania.
Wakati huo huo shirika la Umoja wa Ulaya linaloshughulikia udhibiti wa mipaka Frontex limesema kuwa litaisadia Italia katika kukabiliana na wimbi la wakimbizi kutoka Afrika kaskazini wanaoingia katika nchi hiyo kinyume na sheria.Mkuu wa shirika hilo Laitinen amesema kuwa asasi hiyo itapeleka hivi punde maafisa hadi 50 na vyombo vya usafiri wa baharini pamoja na ndege.
Maafisa wa Italia waliulaumu Umoja wa Ulaya kwa kuchelewa kuchukua za kuwashughulikia wakimbizi kutoka Afrika ya Kaskazini.