1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yarejea katika Baraza la Usalama

John Juma DPAE, APE
3 Januari 2019

Ujerumani ambayo imerejea katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuwa nje ya baraza hilo kwa miaka miwili imesema inataka kutumia uwepo wake kutafuta masuluhisho kwa mizozo inayozonga ulimwengu.

UN Sicherheitsrat Yemen
Picha: Reuters/C. Allegri

Ujerumani imerejea tena katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kama mwanachama asiye wa kudumu. Ujerumani imekuwa nje ya baraza hilo kwa muda wa miaka sita.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepata nchi tano ambazo ni wanachama wapya wasio wa kudumu: Ujerumani, Ubelgiji, Indonesia, Afrika ya Kusini na Jamhuri ya Dominica. Sawa na wanachama wengine wasio wa kudumu, Ujerumani itahudumu katika baraza hilo kwa muda wa miaka miwili.

Yatakayojadiliwa mwezi huu wa Januari

Balozi wa kudumu wa Jamhuri ya Dominika katika Umoja wa Mataifa, ambaye nchi yake ndiyo kwa sasa inashikilia nafasi ya urais wa kubadilishana wa baraza hilo, Jose Singer amewaambia waandishi habari kuwa, mwezi huu, baraza hilo litajadli migogoro ya Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Syria, Mali, Libya, Cyprus na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Balozi Singer pia amezungumzia uwezekano wa kukutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas:

"Kuhusu mkutano na Abbas, nitafurahi ikiwa atakuwa hapa tarehe 15 ambapo kutakuwa na mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Mara ya mwisho Ujerumani ilikuwa mwanachama asiye wa kudumu katika Baraza hilo ni mwaka 2011 na 2012.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas.Picha: picture-alliance/R. Drew

Mnamo siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas, alisema nchi yake inataka kujihusisha zaidi kupata masuluhisho ya mizozo ya ulimwengu kwa kutumia nafasi yake katika baraza hilo.

Masuala ya Ujerumani katika Ajenda ya Baraza la Usalama

Maas aliongeza kuwa Ujerumani inataka kuweka masuala yake katika ajenda za baraza hilo huku akitoa mfano kuwa baraza la usalama sharti lishughulikie suala la mabadiliko ya tabia nchi kama tatizo la kiusalama katika maeneo mengi ulimwenguni.

Masuala mengine ambayo Ujerumani inataka kupewa kipaumbele ni wanawake kupewa nafasi zaidi katika kuzuia na kudhibiti mizozo, wanawake na wasichana wakingwe vya kutosha dhidi ya dhuluma za ngono, kuimarishwa kwa sheria ya kimataifa kuhusu uzingatifu wa utu na watoaji misaada ya kiutu walindwe vyema.

Nguvu mpya katika kupambana na silaha za nyuklia

Heiko Maas alisema pia kuwa Ujerumani vilevile inapanga kuongeza nguvu mpya kuhusu suala gumu la kuachana na silaha za nyuklia na udhibiti wa silaha.

Baraza hilo lenye nguvu zaidi na lililo na jumla ya nchi wanachama 15, lina nchi tano zinazoshikilia viti vya kudumu na zina kura za turufu, nazo ni Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa na China.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW