Ujerumani yasema EU huenda ikachukua hatua iwapo Urusi haitobadili msimamo wake
11 Machi 2014Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema iwapo wiki itapita kabla ya Urusi kubadilisha tabia yake, basi siku ya Jumatatu wiki Ijayo, kikao cha baraza la Umoja wa Ulaya kitabidi kujadili hatua za kuchukua dhidi ya Urusi.
Frank-Walter Steinmeier aliyazungumza hayo katika ziara yake aliyoifanya kwenye mataifa ya Baltic, ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya walio na wasiwasi juu ya hali ilivyo nchini Ukraine.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius ameonya kuwa vikwazo dhidi ya Urusi vinaweza kuwekwa mapema wiki hii iwapo Urusi haitakubaliana na matakwa ya mataifa ya Magharibi ya kutafuta suluhu ya mzozo wa Ukraine.
Vikwazo hivyo vinajumuisha kuzuwiya mali binafsi za raia wa Urusi au Ukraine wanaoaminika kuchochea ghasia na pia kuwanyima visa za kusafiria.
Aidha Fabius amesema iwapo Urusi itakubaliana na matakwa ya mataifa ya Magharibi, basi waziri mwenzake John Kerry wa Marekani atasafiri kuelekea Moscow na vikwazo huenda visiwekwe haraka.
Viktor Yanoukovich asema bado yeye ni rais halali
Huku hayo yakiarifiwa Rais aliyeondolewa madarakani Viktor Yanoukovich aliyejitokeza hadharani leo kwa mara ya kwanza tangu kipindi cha wiki moja amesisitiza kwamba bado anabakia kuwa rais halali wa nchi hiyo na mkuu wa majeshi huku akisema ana imani wanajeshi wake hawawezi kukubali amri yoyote ya kutekeleza uhalifu.
Katika taarifa aliyoitowa kusini mwa Urusi katika mji wa Rostov-on-Don, Yanukovich alisema wanazi mambo leo wamechukua madaraka katika mji mkuu wa Ukraine Kiev. Amesema uchaguzi wa Urais uliopangiwa kufanyika May 25 mwaka huu si wa halali.
Kwa sasa wanajeshi wa Urusi wamezingira rasi ya Crimea, ambayo inajitayarisha kupiga kura ya maoni jumapili ijayo kuamua iwapo ijiunge na taifa la Urusi au ibakie kuwa ndani ya Ukraine.
Wakati huo huo Rais wa Marekani Barrack Obama na washirika wake wa Ulaya wanaihimiza Urusi kuondoa wanajeshi wake katika Rasi ya Crimea na kuanza majadiliano ya haraka na utawala mpya wa Ukraine ambao awali Putin alisema ulichukua madaraka kupitia njia ya mapinduzi isiokubalika kikatiba.
Waziri Mkuu kuelekea Marekani kujadili msaada wa fedha kwa Ukraine
Haya yanatokea wakati waziri mkuu mpya wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akijiandaa kuelekea Marekani kuzungumza na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Waziri Mkuu Yatsenyuk pia atakuwa na mkutano wake wa kwanza na rais Barrack Obama, kuzungumzia msaada wa kifedha kwa Ukraine.
Kwa upande mwengine Jumuiya ya kujihami ya NATO imetangaza kuwa itapeleka ndege za uchunguzi nchini Poland na Romania kufuatilia hali halisi ya mambo katika mgogoro wa Ukraine.
Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri Yusuf Saumu