Ujerumani yasema haitoshiriki mashambulizi dhidi ya Iran
2 Machi 2026
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul, amesema Berlin haitoshiriki mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, mnamo wakati mzozo wa Mashariki ya Kati ukizidi kusambaa. Wadephul, amesema serikali ya Ujerumani, haina lengo la kujiunga na mashambulizi hayo, ikiwa ni siku mbili tu baada ya Israel na Marekani kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran siku ya Jumamosi.
Wadephul, alikuwa akizungumza na kituo cha radio cha Ujerumani, Deutschlandfunk, na kuongeza kwamba nchi hiyo haina rasilimali muhimu za kijeshi, lakini wanajeshi wake watajilinda endapo watashambuliwa.
Tofauti na Uingereza, ambayo inairuhusu Marekani kutumia kambi zake katika eneo hilo kuharibu makombora ya Iran, Ujerumani haina kambi za kijeshi katika eneo hilo, lakini imekuwa na vikosi kutoka jeshi la Ujerumani la Bundeswehr, katika nchi za Jordan na Iraq.