Ujerumani yasema iko tayari kuchangia ujenzi wa Syria mpya
14 Septemba 2018Kauli hiyo ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas inaonekana kama inalijibu ombi la Rais wa Urusi Vladimir Putin la mwezi uliopita alipotaka bara la Ulaya lishiriki katika ujenzi wa Syria mpya. Wakati huo huo, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameisisitizia Urusi kutumia ushawishi wake ili kumshawishi rais wa Syria Bashar al-Assad aahirisha operesheni ya kijeshi katika maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani katika jimbo la Idlib.
Vikosi vya serikali ya Syria vinavyosaidiwa na Urusi vimeuzunguuka mji wa Idlib katika wiki za hivi karibuni, huku kukiwa na hofu ya kufanyika mashambulio ya ardhini na ya anga katika juhudi za kuliteka eneo hilo la mwisho linaloshikiliwa na wapinzani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema serikali ya Syria haijitayarishi kufanya operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya wapinzani wa Idlib akiongeza kuwa Urusi itafanya kila kitu kulinda usalama wa raia.
Taarifa za hivi punde zinatufahamisha kuwa afisa mmoja mkuu wa Uturuki amehakikisha kuwa nchi yake imeimarisha ulinzi katika vizuizi vya usalama 12 vilivyo karibu ya Idlib wakati ambapo jeshi la Syria linajiandaa kufanya mashambulizi ya kulikomboa jimbo hilo.
Mratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mgogoro wa Syria Panos Moumtiz amesema Umoja wa Mataifa umeweka vifaa vya GPS katika maeneo 235 katika jimbo la Idlib, ikiwa ni katika shule na hospitali, kutokana na hofu ya mashambulio ya kijeshi. Amesema bado wanatafakari endapo hali mbaya zaidi itatokea.
Wanaharakati wa Syria wamesema msururu wa wanajeshi wa Uturuki uliingia Syria kupitia kivuko cha Kfar Lusin kaskazini mwa Idlib. Magari ya kivita na askari wenye bunduki na mizinga wameonekana katika barabara za Idlib. Uturuki imepeleka mamia ya askari hao kufuatia makubaliano mapya yaliyofikiwa mwaka jana pamoja na Urusi na Iran.
Kwa mujibu wa ikulu ya Urusi nchi hiyo inaandaa mkutano kati ya marais Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Jumatatu ijayo. Mkutano huo utafanyika katika mji wa kusini mwa Urusi wa Sochi huku vita vya nchini Syria vikiwa ajenda kuu ya mazungumzo ya viongozi hao.
Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa shirika la habari la Urusi TASS kuhusu maandalizi ya mkutano huo. Urusi na Uturuki zinaunga mkono pande tofauti katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.
Umoja wa Mataifa umeonya mashambulio dhidi ya jimbo la Idlib yanaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika karne hii na pia kusabisha idadi ya maelfu ya wakimbizi.
Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/AP/DPA/
Mhariri: Gakuba, Daniel