1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasema Navalny alipewa sumu ya Novichok

3 Septemba 2020

Viongozi kutoka kote ulimwenguni wamelaani tukio la kupewa sumu kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny katika jaribio la kutaka kumuuwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anatarajia Urusi kueleza msimamo wake

Russland Moskau | Alexej Nawalny, Oppositionspolitiker
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Golovkin

Kansela Merkel amesema kulikuwa na "habari za kutisha” zilizoonesha "bila shaka yoyote" kuwa tukio la kupewa sumu Alexei Navalny lilikuwa "jaribio la mauaji kwa kutumia sumu inayoathiri mishipa ya fahamu” baada ya vipimo vya nchini Ujerumani kuonyesha kuwa sumu ya Novichok ilitumika dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani. Merkel amesema Navalny ni "muhanga wa uhalifu ulionuia kumnyamazisha,” akiongeza kuwa ukubwa wa suala hilo ni muhimu kwake "kuchukua msimamo wa wazi”. Hatima ya Alexei Navalny imevutia hisia za ulimwengu wote. Ulimwengu utasubiri majibu. Tutawafahamisha washirika wetu wa EU na NATO kuhusu matokeo haya ya uchunguzi. Tutashauriana na kuamua hatua mwafaka ya pamoja tutakayochukua kwa kutegemea na kuhusika kwa Urusi. Uhalifu dhidi ya Alexei Navalny ni kinyume na maadili na haki za msingi tunazozilinda.

Merkel amesema kisa hicho kinaibua maswali muhimu sana ambayo ni serikali ya Urusi pekee inayoweza kujibu. Vipimo hivyo vilifanywa katika maabara maalum ya jeshi la Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas mapema jana alimuita balozi wa Urusi Berlin kujadili hali hiyo.

Navalny anatibiwa Berlin chini ya ulinzi mkali wa polisiPicha: Getty Images/S. Gallup

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amelaani kitendo hicho alichokiita cha kuchukiza na cha woga. Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Ullyot amesema kitendo hicho ni cha kukemewa kabisa na kuwa watashirikiana na washirika ili kuwawajibisha waliohusika nchini Urusi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema amefadhaishwa na ufichuzi huo na akalaani matumizi ya bila kujali ya sumu ya aina hiyo. Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema Urusi lazima ifanye uchunguzi kamili na wa uwazi. Katibu Mkuu Jens Stolltenberg amesema NATO itashauriana na Ujerumani na washirika wake wote kuhusu hatua za kuchukua.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelinganisha kisa hicho na cha jasusi wa zamani wa Urusi aliyekimbilia Uingereza Sergei Skripal, akisema kuwa Uingereza itashikiana na washirika wa kimataifa kuhakikisha haki inatendeka kwa Navalny. Katika tukio la Skripal, karibu washirika 30 wa Magharibi waliwafurusha nchini mwao wanadiplomasia wa Urusi

Katika kujibu matokeo hayo, msemji wa Putin Dmitry Peskov alisema mamlaka za Urusi ziko tayari kushirikiana kikamilifu na Ujerumani katika kisa hicho.

Navalny mwenye umri wa miaka 44 ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi Vladmir Putin. Navalny aliwahi kudai kuwa alipewa sumu wakati mmoja akiwa kizuizini Moscow mwaka jana. Aliwahi pia kushambuliwa hadharani. Alisafirishwa Berlin kwa matibabu Agosti 22, siku mbili baada ya kuugua kwa ghafla akiwa kwenye ndege nchini Urusi.

reuters, ap, afp, dpa