Ujerumani yashindwa kurejesha wahamiaji wengi waliokataliwa
7 Machi 2026
Takriban theluthi mbili ya mipango ya kuwarejesha wahamiaji kutoka Ujerumani ilishindikana kutekelezwa mwaka uliopita, kulingana na takwimu mpya zilizochochea wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi na wanasiasa wa kihafidhina.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, jumla ya watu 22,787 walirejeshwa kwa mafanikio huku 32,855 wakishindwa kurejeshwa kabla hawajakabidhiwa kwa maafisa wa uhamiaji katika viwanja vya ndege, polisi walilithibitishia shirika la habari la dpa siku ya Jumamosi.
Sababu kubwa ya kushindikana kwa operesheni hizo ilikuwa kushindwa kwa polisi wa majimbo mbalimbali kuwakamata au kuwafikisha wahusika bila taarifa ya awali. Hali hiyo iliathiri watu 21,341.
Katika visa 11,184, maombi ya kurejesha wahamiaji yalifutwa kabisa kabla ya utekelezaji.
Aidha, majaribio 1,593 ya kurejesha wahamiaji yalishindikana baada ya wahusika tayari kukabidhiwa kwa maafisa katika viwanja vya ndege.
Wanasiasa wataka hatua kali zaidi
Takwimu hizo zimeibua mjadala mpya wa kisiasa kuhusu namna ya kupunguza idadi ya operesheni za kurejesha wahamiaji zinazoshindikana.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Hesse, Roman Poseck, alipendekeza matumizi ya teknolojia ya kufuatilia simu za mkononi za watu waliotakiwa kuondoka nchini lakini hawapatikani.
Akizungumza na gazeti la Die Welt, Poseck alisema hatua hiyo hailengi kuweka watu wote chini ya ufuatiliaji wa jumla.
Alisema teknolojia hiyo ingetumika tu katika hali ambapo mtu anayepaswa kuondoka nchini hawezi kupatikana.
Kwa mujibu wake, lengo ni kuwatafuta haraka na kuhakikisha wanaondolewa nchini kwa mujibu wa sheria.
Wito wa kurejesha vituo vya kuwazuilia wahamiaji
Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Saxony, Armin Schuster, ambaye pia anatoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU, aliunga mkono wazo la kufuatilia simu za mkononi.
Alisema ufuatiliaji wa simu unaweza kuwa nyongeza muhimu kwa zana zilizopo za kutekeleza urejeshaji.
Hata hivyo, Schuster alisisitiza kuwa itakuwa bora zaidi kama watu wanaotakiwa kuondoka nchini hawatapewa nafasi ya kujificha tangu mwanzo.
Kwa sababu hiyo, alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya (EU) kuruhusu tena matumizi ya vituo maalum vya kuwazuilia watu wanaosubiri kurejeshwa katika nchi zao.
Hatua hiyo, alisema, inaweza kusaidia kuhakikisha utekelezaji wa maamuzi ya kuwarejesha wahamiaji unafanyika kwa ufanisi zaidi.