Ujerumani yatangaza serikali mpya
16 Desemba 2013Chama cha Lugha cha Ujerumani kimeipa jina kwa ufupi serikali hiyo "GroKo" yaani muungano mkuu wa serikali ya mseto inayojumuisha vyama ndugu vya kihafidhina cha CDU na CSU na kile cha Social Demokratik SPD.
Kwa mara ya kwanza katika historia chama cha upinzani cha SPD ambacho kilishindwa katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliofanyika hapo mwezi wa Septemba kiliwataka wanachama wake wapige kura kuridhia chama hicho kujiunga katika serikali ya mseto chini ya uongozi wa Kansela Angela Merkel ambacho chama chake kilishinda katika uchaguzi mkuu huo.Matokeo ya kura hiyo ingelikuwa ya "hapana" ingelibidi kufanyike mazungumzo mapya ya kuundwa kwa serikali hiyo ya mseto.
Katika ngazi ya kitaifa ya serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kulikuwako mara mbili kwa serikali za muungano mkuu.Kwa mara ya kwanza serikali hiyo iliundwa kati ya vyama ndugu vya CDU/CSU na chama cha SPD hapo mwaka 1966.Mara ya pili serikali hiyo ya muungano mkuu iliundwa hapo mwaka 2005 hadi 2009 na kuungozwa na Kansela Angela Merkel.
Mawaziri wa CDU
Katika baraza hili jipya la mawaziri waziri wa kazi Ursula von der Leyen anakuwa waziri wa Ulinzi wadhifa anaouchukuwa kutoka kwa alieyekuwa waziri wa wizara hiyo Thomas de Maziere ambaye sasa anakuwa waziri wa mambo ya ndani wadhifa ambao aliwahi kuushikilia mwaka 2009 hadi mwaka 2011.
Chama hicho cha CDU pia kinashika wadhifa wa mawaziri wengine watatu ambapo Wolfgang Schaeuble ataendelea kuwa waziri wa fedha,Johanna Wanka ataendelea kuwa waziri wa elimu na utafiti wakati Hermann Groehe atakuwa waziri wa afya.
Mwaziri walioteuliwa na chama ndugu cha CSU ni pamoja na Alexander Dobrihndt anayekuwa waziri wa uchukuzi na miundo mbinu ya digitali na waziri wa mambo ya ndani Hans- Peter Friedrich anabadilishana nafasi na waziri wa kilimo Gerd Mueller.
Mawaziri wa SPD
Hapo jana chama cha SPD kilitangulia kutangaza mawaziri wake sita ambapo mwenyekiti wa chama hicho Sigmar Gabriel anakuwa naibu kansela na waziri wa "wizara kuu" inayochanganya uchumi na nishati na Walter Steimeir amerudia tena kuwa waziri wa mambo ya nje.
Everhard Holtmann Mkurugenzi wa Utafiti katika Kituo cha Utafiti wa Jamii Chuo Kikuu cha Halle- Wittenberg amesema serikali ya muungano mkuu ya mwaka 2005 hadi mwaka 2009 ilifanya kazi nzuri ya kuweza kukabiliana na mzozo wa kiuchumi na kifedha duniani.
Jambo ambalo anasema linaonyesha ufanisi ya serikali ya mseto ya muungano mkuu. Ameongeza kusema kwamba serikali za muungano mkuu zinaweza kufanikisha mengi kwa Wajerumani.
Vyama vya CDU/CSU na SPD vinatazamaiwa kusaini makubaliano ya kurasa 185 ya kuundwa kwa serikali hiyo ya mmungano mkuu ambayo ni ya tatu katika historia ya Ujerumani leo hii.
Mwandishi :Christina Carla Bleiker/Mohamed Dahman/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef