1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatikiswa na mgomo mkubwa wa sekta ya usafiri

27 Machi 2023

Safari chungunzima za ndege zimefutwa katika viwanja vya ndege Ujerumani na vituo vya matreni wasafiri wajikuta wakihangaika. Shughuli nyingi zaathirika kutokana na kukosekana usafiri

Deutschland Bundesweiter Streik im Verkehr hat begonnen | HBF München
Picha: Lukas Barth/REUTERS

Ujerumani imekumbwa na mgomo mkubwa kabisa wa usafiri wa umma hii leo,wafanyakazi wa huduma za usafiri wakidai nyongeza za mshahara.

Mgomo katika sekta ya usafiri wa umma nchini Ujerumani umeanza tangu saa sita usiku wa kuamkia leo na sehemu kubwa ya nchi shughuli zimeathirika kutokana na mgomo huo uliotishwa na vyama vya wafanyakazi Verdi na EVG.

Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Ni mgomo unaotarajiwa kutikisa nchi kwa masaa 24 hii leo ikihusisha mgomo wa wafanyakazi katika mifumo yote ya usafiri tangu  viwanja vya ndege,bandari, treni za mwendo kasi ,mabasi na  treni za chini kwa chini.

Kutokana na hali ngumu ya maisha kufuatia mfumko wa bei, Chama cha kutetea maslahi ya wafanyakazi  nchini Ujerumani Verdi kinadai nyongeza ya asilimia 10.5 kwa wafanyakazi hao wakati EVG  kikitaka wafanyakazi inaowawakilisha waongezewa asilimia 12.

Waajiri lakini  katika sekta hiyo ambayo kwa sehemu kubwa ni mashirika ya serikali na ya umma mpaka sasa wamekataa kutimiza madai ya vyama hivyo,  na badala yake wameridhia kutoa nyongeza ya asilimia 5 pamoja na malipo ya yuro 1000 za ziada mwaka huu, na 1500 mwaka ujao zitakazotolewa mara moja tu.

Kufuatia kukosekana maelewano kati ya pande hizo nchi nzima hii leo kunashuhudia athari za mgomo huo ikitajwa kwamba  hakuna shughuli zozote za usafiri zinazofanyika katika vituo vikuu mbali mbali vya usafiri wa Treni katika majimbo mengi ya nchi.

Picha: Jana Rodenbusch/REUTERS

Safari chungunzima za ndege zimefutwa kwenye viwanja mbali mbali ikiwemo viwanja vikubwa kabisa  vya ndege Ujerumani Frankfurt na Munich.

Ili kuepusha pengo katika usambazaji wa bidhaa nchini jana Jumapili waziri wa uchukuzi Volker Wissing aliyaamrisha majimbo kuondowa vizuizi dhidi ya malori ya kuingiza bidhaa wakati pia akiziomba mamlaka za viwanja vya ndege  kuruhusu ndege kuondoka na kutuwa Jumapili usiku ili wasafiri waliokuwa wakihangaika kuendelea na safari zao walizokuwa wamekwishazipanga.

Ikumbukwe kwamba chama cha wafanyakazi Verdi kinawakilisha kiasi wafanyakazi milioni 2.5 katika sekta ya usafiri wa umma wakati kile cha EVG kinawakilisha wafanyakazi 230,000 wa usafiri wa treni na mabasi.

Frank Werneke ambaye ni mkuu wa Verdi amekiri kwamba athari kubwa zitashuhudiwa kutokana na mgomo huu lakini akaongeza kusema kwamba mapambano ya wafanyakazi hayawezi kuzaa matunda ikiwa athari zake hazionekani.

Picha: Lukas Barth/REUTERS

Kwa mtazamo wake amesema ni bora kushuhudiwa mgomo mkubwa wa nchi nzima kwa siku moja,utakaowaletea tija kuliko kuandaa migomo ya kila wiki ambayo haina matokeo.

Kama inavyoshuhudiwa katika nchi nyingine nyingi,watu nchini Ujerumani wanahangaika kutokana na mfumko wa bei uliofikia asilimia 8.7 kufikia mwezi Februari  baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kusababisha gharama za vyakula na nishati  kupanda kwa namna ambayo haijapata kutokea.

Mgomo huu ndio mkubwa zaidi kuwahi kuonekana kwenye sekta ya usafiri wa umma nchi ujerumani kwa kipindi cha miongo kadhaa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW