1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatishia kuiwekea vikwazo Urusi kuhusu Navalny

Sylvia Mwehozi
6 Septemba 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema, Berlin itajadili suala la kuiwekea vikwazo Urusi kuhusiana na tukio la kumlisha sumu kiongozi wa upinzani Alexai Navalny, ikiwa Kremlin haitotoa maelezo ya kina

Russland Alexej Nawalny
Picha: Reuters/S. Zhumatov

Kiongozi wa upinzani wa Urusi na mwanaharakati wa kupinga ufisadi Navalny, aliumwa mwezi uliopita na kutibiwa nchini Siberia kabla ya kukimbizwa mjini Berlin. Wiki iliyopita, Ujerumani ilisema kulikuwa na "ushahidi wa wazi" kuwa mpinzani huyo wa rais Vladmir Putin alipewa sumu ya Novichok.

Maas amelieleza gazeti la kila siku la Ujerumani Bild kwamba "tuna matarajio makubwa kwa serikali ya Urusi kutatua uhalifu huu mkubwa", akiongeza kuwa "ikiwa serikali haihusiki na shambulio hilo, basi ni wajibu wake kusema ukweli."

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: Reuters/S. Loos

Maas amedai kuwa kama Urusi haitosaidia katika kutoa ufafanuzi wa kilichotokea katika siku zijazo, Ujerumani italazimika kujadili hatua za kuchukua na washirika wake.

Kulingana na Mwanadiplomasia huyo, uhalifu dhidi ya Navalny ni ukiukaji wa mkataba wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za kemikali na lazima kuwe na jibu linalofaa, "tunapofikiria juu ya vikwazo vinapaswa kuwekwa haraka iwezekanavyo"

Viongozi wa mataifa ya Magharibi na Warusi wengi wameelezea hofu ya kile washirika wa Navalny wanasema ni matumizi ya kwanza ya kemikali  dhidi ya kiongozi wa ngazi ya juu wa upinzani katika ardhi ya Urusi.

Kremlin inakana kuhusika

Navalny hatimaye asafirishwa Ujerumani kwa matibabu zaidiUrusi yenyewe imekana kuhusika na shambulio hilo na waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov amesema Ujerumani imeshindwa kutoa ushahidi wowote kwa waendesha mashitaka wa Moscow. Msemaji wa wizara hiyo Maria Zakharova hapo Jumapili aliituhumu Ujerumani kwa kukwamisha juhudi za uchunguzi wa kesi ya Navalny.

"Berlin inazuia mchakato wa uchunguzi ambao imeuitisha. Kwa makusudi?" aliandika Zakharova katika ukurasa wa Facebook. "Kama serikali ya Ujerumani inasema kweli kwenye taarifa zake basi itatakiwa kujibu kwa haraka maombi ya ofisi ya mwendesha mashitaka wa Urusi", alimalizia Zakharova.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic RaabPicha: picture-alliance/Photoshot/UPPA/Avalon/J. Ng

Viashiria kadhaa

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas, kuna viashiria kadhaa kwamba Urusi ilihusika na shambulio la sumu, katika shutuma kali kutoka kwa Ujerumani. "Ni idadi ndogo ya watu wanaoweza kuifikia Novichok na sumu hii ilitumiwa na idara za kijasusi za Urusi katika shambulio dhidi ya afisa wa zamani wa usalama Sergei Skripal", akimaanisha shambulio la 2018 la afisa huyo na binti yake katika mji wa Salisbury huko Uingereza.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab amesema Jumapili  kuwa Urusi lazima ieleze kuhusu vipi kiongozi wa upinzani nchini humo Alexei Navalny alipewa sumu katika kile Ujerumani imesema ni kemikali ya Novichok.

Raab amekiambia kituo cha habari cha Sky kwamba kile kilicho wazi kwasasa ni kwamba serikali ya Urusi ina maswali mengi magumu ya kujibu. Raab ameongeza kuwa iwapo tukio hilo lilihusisha serikali au la, Urusi ina jukumu la kuhakikisha kuwa silaha za kemikali hazitumiwi nchini humo.

 

        

     

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW