1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatoa wito kuongeza juhudi za kumaliza vita Yemen

17 Januari 2019

Waziri wa mamboya nje wa Ujerumani ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongezea juhudi za kumaliza vita  nchini Yemen kwenye mkutano wa kimataifa uliohudhuriwa na wadau wote katika mgogoro wa Yemen.

Jemen - Hafenstadt Hudaida
Picha: picture-alliance/akg/H. Champollion

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas aliongoza mazungumzo mengine mapya kuhusu mchakato wa amani nchini ya Yemeni. Majadiliano hayo yaliyofanyika mjini Berlin yalilenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mazungumzo ya mjini Stockholm yaliyofikiwa mwezi uliopita.Wawakilishi wa serikali 17 na mashirika ya kimataifa walikutana mjini Berlin siku ya Jumatano.

Mkutano huo wa mjini Berlin uliozingatiwa kuwa mdahalo wa ngazi ya juu ulikuwa na lengo la kuendeleza  mafanikio yaliyopatikana kwenye mkutano uliofanyika nchini Sweden. Mkutano huo ulikuwa wa kwanza, tangu mwaka 2016 uliozileta pamoja pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchini Yemen.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas aliwaambia wajumbe kwenye mkutano mjini Berlin kwamba, kwa mara ya kwanza zimepatikana habari njema kutoka Yemen. Waziri Maas amesema hatua muhimu imechukuliwa kwa lengo la kuleta amani nchini humo, ambayo inaweza kuwa msingi katika kuitatua migogoro mingine duniani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/AA/A. Hosbas

Maas, ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughgulikia mgogoro wa Yemen Martin Griffiths. Vita vya nchini Yemen vilianza mnamo mwaka 2014 baada ya waasi wa Kihouthi kuiteka sehemu kubwa ya nchi na kuidhibiti, ikiwa pamoja a mji mkuu wa nchi  hiyo Sanaa.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amearifu kwamba makubaliano ya kusimamisha mapigano kwenye mji wa Hodeida kwa ujumla yanaendelea kutekelezwa na kwamba sasa Umoja wa Mataifa umeweka waangalizi wake kwenye mji huo. Mjumbe huyo pia  amesisitiza imani kubwa juu ya kamati ya kimataifa inayosimamia utekelezwaji wa makubaliano ya kusimamisha mapigano katika mji huo.

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Yemen Khalid Al Yamani ameliambia shirika la habari la Reuters  kwamba wapiganaji wa Kihouthi bado hawajatulia kabisa katika mji wa Hodeida.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Yemen Martin Griffiths Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Lakini walipozungumza na waandishi wa habari kabla ya mkutano kuanza, si waziri Maas, bwana Griffiths, au mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Lise Grande, aliyejibu mswali kuhusu kwa nini hakuna wawakilishi wa Yemeni waliokuwa kwenye mkutano huo?

Wakati huo huo, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Lise Grande amesema, hali ya kibinadamu nchini Yemen bado ni mbaya mno. Amesema watu zaidi ya milioni 10 kila wanapoamka asubuhi huwa hawajui kabisa jinsi watakavyopata chakula.

Umoja wa Mataifa umesema kusitishwa kwa mapigano kumetoa fursa ya utoaji wa chakula katika maeneo mawili nchini Yemen kwa mara ya kwanza katika miezi sita.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas pia ametangaza kuwa Ujerumani itachangia Euro milioni 4.5 kwenye mfuko wa kusaidia mchakato wa amani ya Yemen. Mkutano wa wafadhili umepangwa kufanyika mjini Geneva mwezi Februari.

Mwandishi:Zainab Aziz/Knight Ben

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW