Ujerumani yataka mageuzi makubwa ya Baraza la Usalama la UN
2 Januari 2026
"Baraza la Usalama lazima liakisi ulimwengu wa karne ya 21 na sio ule wa kipindi cha baada ya vita baada ya 1945," Wadephul aliambia shirika la habari la Ujerumani - dpa, akirudia wito wa awali wa Berlin wa kuwepo mabadiliko.
Ujerumani inagombea kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama mnamo Juni 2026 kwa muhula wa 2027-28.
Baraza hilo linajumuisha nchi 15 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Nchi tano zenye nguvu za nyuklia na washindi wa Vita vya Pili vya Dunia ni wanachama wa kudumu na wana mamlaka ya kura ya turufu juu ya azimio lolote ambalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapiga kura: Marekani, China, Urusi, Uingereza na Ufaransa.
Viti 10 vilivyobaki huwa ni vya mzunguko miongoni mwa nchi nyingine wanachama kila baada ya miaka miwili.
Indo-Pasifiki, Afrika na Amerika Kusini kupewa nafasi zaidi
Alipoulizwa angefanya nini ili kuisaidia Ujerumani kuipiku Austria na Ureno katika kura ya kiti kisicho cha kudumu, Wadephul alisema: "Nikizungumza kwa lugha ya soka, ningesema tunapaswa kuwa tayari kucheza katika kila nafasi kwa ajili ya washirika wetu wa kimataifa."
Alipozungumzia suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Wadephul alisema Ujerumani inashirikiana na nchi ndogo za visiwa kuunda sera ya kigeni inayozingatia hali ya hewa ambayo ilizingatia changamoto mahususi za kuwepo kwa nchi hizo.
Aliongeza kuwa kutatafutwa ushirikiano wa kimataifa ambao utaimarishwa upya, 2026.
"Kufuatia ushirikiano mkubwa barani Ulaya na Asia, kanda ya Indo-Pasifiki, Afrika na Amerika Kusini sasa zitakuwa sehemu ya hilo," waziri huyo alisema.
Wadephul aidha alisema licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia kuonyesha, kupitia azimio lake linalounga mkono mpango wa amani wa Mashariki ya Kati, kwamba lina uwezo wa kufanya kazi, bado serikali ya Ujerumani inaamini kwamba chombo hicho bado kinahitaji mageuzi makubwa, yenye wigo wa kurahisisha baadhi ya masuala.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema mwishoni mwa Novemba, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika nchini Angola, kwamba anaunga mkono wito wa viti viwili vya kudumu vya Afrika katika Baraza la UsalamaMerz alisema Ulaya na Afrika kwa pamoja zina zaidi ya asilimia 40 ya kura zote katika Umoja wa Mataifa.
"Pamoja, tuna nguvu kubwa," Merz alisema. "Lakini kwa ajili hiyo, Afrika lazima pia iwakilishwe vyema kimataifa, kwa njia inayoakisi uzito wa bara hili."