Ujerumani na matumaini ya kukidhibiti kirusi cha Omicron
8 Februari 2022Mkuu wa Taasisi ya udhibiti wa magonjwa nchini Ujerumani ya Robert Koch, Lothar Wieler, amewaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba ana matumaini juu ya wimbi la maambukizi ya virusi vya corona aina ya Omicron litadhibitiwa hivi karibuni.
Wieler amesema kama ilivyo katika nchi nyingine nyingi, kirusi cha Omicron kiachoambukiza kwa kasi kimesababisha kuongezeka kwa idadi ya watu walioambukizwa katika wiki za hivi karibuni.
Taasisi ya RKI imeorodhesha watu milioni 1.2 walioambukizwa katikia kipindi cha siku saba zilizopita,hii ni takriban asilimia10 ya watu walioambukizwa nchini Ujerumani kote hadi sasa. Wieler amebainisha kuwa kirusi cha Omicron kinaongoza kuwa ni sababu ya watu kulazwa hospitalini kuliko kirusi cha Delta.
Waziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach amekilaumu chama kikuu cha upinzani kwa kutoa mwito wa kusitisha utekelezaji wa lazima kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kupata chanjo ya COVID-19. Waziri wa afya wa Ujerumani amesema hii inaweza kutoa ishara ya isiyo sahihi. Waziri Lauterbach pia ametoa tahadhari kutokana na wito wa wanasiasa wanaotaka hali ya sasa ya vikwazo vya corona iondolewe nchini Ujerumani.
Ufaransa inajiandaa kuiondoa sheria iliyowalazimisha wasafiri waliochanjwa kutoka nje ya Umoja wa Ulaya kuwa na cheti kinachowaonesha hawana maambukizi ya Covid-19. Hatua hiyo imefikiwa baada ya idadi ya maambukizo ya kila siku kuendelea kupungua nchini humo.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ametaka kusitishwa kwa maandamano ya mamia ya madereva wa malori wanaopinga vizuizi vya Covid-19. Maandamano hayo yamesababisha kusimama kwa shughuli katika mji mkuu wa Canada, Ottawa kwa siku ya 11 kufikia leo tarehe 08.02.2022.
Huko nchini New Zealand msafara wa malori umefunga ya mitaa karibu na bunge la nchi hiyo katika mji wa Wellington katika maandamano ya kupinga chanjo ya Covid-19 yaliyochochewa na maandamano ya nchini Canada.
Huko nchini Uganda inatarajia kuweka sheria itakayosimamia uagizaji wa chanjo. Rasimu hiyo ya sheria inalenga kukuza msukumo wa kuwachanja watu zaidi dhidiu ya Covid-19 katika nchi hiyo ya Mashariki mwa Afrika.
Muswada huo uliopendekezwa, unaweza kufanyiwa mabadiliko iwapo kamati ya afya ya bunge itapendekeza pindi itakapokamilisha uchunguzi wake. Muswada huo unapendekeza kifungo cha hadi miezi sita jela kwa yeyote atakayekiuka maelekezo ya chanjo wakati milipuko ya magonjwa.
Hata hivyo juhudi za maafisa wa Uganda katika miezi ya hivi karibuni kutekeleza amri za lazima kuhusiana na chanjo hazikufanikiwa. Pendekezo la ulazima wa chanjo kwa watu ndipo waweze kutumia usafiri wa umma lilikabiliwa na upinzanimkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya usafiri. Mataifa ya Afrika kama Zimbabwe na Ghana yametangaza kuwa ni lazima kupata chanjo kwa wafanyakazi wa sekta za umma.
Vyanzo: DPA/AP/AFP