1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakemea wimbi la wahamiaji wanaoingia Poland

9 Novemba 2021

Ujerumani imeutaka Umoja wa Ulaya kuchukua hatua na kuwazuia wahamiaji haramu wanaovuka mpaka wa Belarus na kuingia Poland, ambao wanatawrajiwa kuongezeka siku za usoni.

Belarus Migranten im Grenzgebiet zu Polen
Picha: Leonid Shcheglov/ITAR-TASS/imago images

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amesema Ujerumani na Poland pekee haziwezi kulishughulikia suala hilo na kuutaka Umoja wa Ulaya kwa jumla kusiamama nao pamoja.

Ombi hilo la Ujerumani limetolewa baada ya Poland kusema kwamba imezuia mamia ya wahamiaji kutoka Belarus waliotaka kuingia nchini humo.

Poland imeonya kwamba maelfu wengine wako njiani, na wakiwasili itatumia silaha kuwazuia kuingia nchini humo.

Soma zaidi: Poland yakosolewa kuwarejesha wakimbizi kinyume cha sheria

Ujerumani imesema inaunga mkono uamuzi wa Poland wa kutaka kujenga ukuta kwenye mpaka wake na Belarus. Seehofer ameliambia gazeti la Bild kwamba haungi mkono utumiaji wa silaha, lakini anakubaliana na uamuzi wa Poland wa kutaka kulinda mipaka yake.

Umoja wa Ulaya unamshutumu rais wa Belarus Alexander Lukashenko kwa kuwasafirisha wahamiaji hao haramu kutoka Mashariki ya Kati na Afrika hadi mjini Minsk, na baadae kuwaruhusu kuvuka mipaka ya kuingilia nchi kama Poland, Luthiania na Latvia.

Wahamiaji wanaovuka mpaka wa Belarus wa kuingilia PolandPicha: Leonid Shcheglov/ITAR-TASS/imago images

Aidha Umoja wa Ulaya umesema Lukashenko anafanya hivyo kulipiza kisasi kwa vikwazo alivyowekewa kwa kosa la kukandamiza upinzani nchini mwake.

Hata hivyo Lukashenko amekana shutuma hizo.

Soma zaidi: Walioteswa Belarus wamshtaki Lukashenko Ujerumani

Wengi wa wahamiaji hao wanaotaka kuingia Poland wanakimbia vita na umaskini katika mataifa ya Mashariki ya Kati.

Wanasema hawana pakwenda kwani Belarus imewazuia kwenda mjini Minsk ili kupanda ndege za kuwarejesha walipotoka, wakati Poland imegoma kuwaruhusu kuingia nchini mwake na kuwapatia hifadhi ya ukimbizi.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amezitolea wito nchi wanachama wa umoja huo kuiwekea vikwazo zaidi Belarus kwa kuruhusu wahamiaji haramu kuingia Ulaya.

Ameongeza kwamba kuwatumia wahamiaji kwa sababu za kisiasa ni kitu kisichokubalika.

Ujerumani kama jirani wa Poland, imeshuhudia ongezeko la wahamiaji haramu wanaoingia nchini humo.

Wahamiaji wanaotokea Belarusi katika eneo la mpaka na PolandPicha: Leonid Shcheglov/BelTA/AP/dpa/picture alliance

Mwezi Oktoba pekee, idadi hiyo ilifika wahamiaji 5,000 kulingana na mamlaka za Ujerumani.

Berlin imeamua kuongeza vituo vya ukaguzi mipakani pamoja na kutuma polisi wa ziada.

Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani, Stephan Mayer, amesema Ujerumani iko tayari kuitumia polisi Poland watakapohitajika.

Mnamo mwaka 2015 hadi 2016, Ujerumani ilipokea wahamiaji wapatao milioni moja na kuwapa hifadhi, lakini tangu wakati huo imebadilisha msimamo wake kuhusu sera ya uhamiaji na hivi sasa hawakaribishwi tena.

Vyanzo: afp