Ujerumani yawasilisha sera za haki za binadamu kwa baraza la haki za binadamu
2 Februari 2009Kamati jumla ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa inayochunguza maswala yote ya haki za binadamu inakutana hii leo mjini Geneva nchini Uswisi kuisikiliza Ujerumani ikiwasilisha sera zake kuhusu haki za binadamu. Wajumbe wa serikali ya Ujerumani wanahudhuria kikao cha kamati hiyo wakiwa na mchanganyiko wa hisia.
Ujerumani kama nchi ya kidemokrasia ambayo imejumulisha ulinzi wa haki za binadamu kwenye katiba yake, haina haja ya kuwa na wasiwasi wa kukosolewa kwa ukiukaji wa haki za binadamu kwenye mkutano huo. Lakini kwa kuwa nchi nyingi wanachama wa baraza la haki za binadamu ni nchi zinazoendelea, Ujerumani inalazimika kujiandaa kujibu maswali magumu kuhusu sera zake za kigeni.
Kamati ya baraza la haki za binadamu ni kama alama mpya ya sera za haki za binadamu za Umoja wa Mataifa - taratibu jumla ya kuchunguza sera za kila nchi mjini Geneva Uswisi. Iwe ni nchi yenye utawala wa kidemokrasia au utawala wa kiimla, kila taifa linatakiwa kusimama mbele ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa na kuelezea hali ya haki za binadamu katika ardhi yake na pia kujibu maswali. Leo ni zamu ya Ujerumani.
Konrad Scharinger, mjumbe wa Ujerumani kwenye mkutano wa mjini Geneva anasema, ''Hapa Ujerumani hali ya haki za binadamu katika miaka iliyopita, imekuwa nzuri. Na ndio maana tunakwenda katika mkutano huu tukijiamini na tukiwa na mtazamo wa kuwa na nafasi nzuri kwenye mkutano huu.''
Ujumbe wa Ujerumani umejiandaa barabara na umewasilisha ripoti ya kina kuhusu hali ya haki za binadamu hapa nchini. Ripoti hiyo inaeleza hatua ambazo Ujerumani imechukua katika kulinda haki za binadamu. Halmashauri kuu ya haki za binadamu ya Ujerumani imewasilisha ripoti yake huku asasi zisizo za kiserikali nazo zikiwa zimefaulu kuwasilisha rasmi ripoti yao.
Nchi zinazoendelea na zinainukia haraka kiuchumi zina idadi kubwa kwenye baraza la haki za binadamu. Nchi hizi zina mtazamo wa kibinafsi kuhusu Ujerumani na nchi nyingine zilizoendelea kiviwanda duniani.
Wolfgang Heinz, mwanachama wa kamati ya wataalamu wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa anasema, ''Nadhani kwa nchi kadhaa za eneo la kusini mada muhimu bila shaka ni zile zinazoyagusa maisha ya raia wao. Maswali yatakayoulizwa yatajumulisha swala la kuwashughulikia wakimbizi, watu waliowasilisha maombi ya ukimbizi. Maswali ya uhamiaji yataulizwa na hiyo ni kwa sababu nzuri. Pia kuna maswala kuhusu ukatili wa polisi na matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa kuwa kumekuwa na mwenendo wa maafisa wa polisi wa nchi za magharibi wanavyowashughulikia raia wa kigeni au wahamiaji ikilinganishwa na raia asili wa mataifa hayo.''
Kwa mara ya kwanza kabisa Ujerumani inakabiliwa na kipimo kikubwa cha kuchunguzwa sera zake kuhusu haki za binadamu kwenye baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Hali hii pengine inahitaji muda kuizowea lakini sio ya kupuuzwa.
Wolfgang Heinz, mwanachama wa kamati ya wataalamu wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa anasema, ''Nadhani ni muhimu kutoanza mazungumzo kuhusu haki za binadamu kwa kusema sisi si kama Uganda, au China au Urusi, bali busara ni kusema tu rahisi kwamba hata hapa kwetu kuna visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na sharti vizingatiwe kwa makini. Lazima kuangalia iwapo kuna habari muhimu, nani wa kubeba dhamana na kipi kinachoweza kuboreshwa. Inapogunduliwa kwa misingi hii kwamba katika kila nchi kuna ukiukaji wa haki za binadamu, ipo haja ya kuongeza juhudi za kulinda haki za binadamu na kujikosoa sisi wenyewe badala ya kuliangalia tatizo hili kuwa la nchi nyingine.''
Utaratibu wa kuzichunguza nchi zote kuhusiana na hali ya haki za binadamu utakapomalizika, kutaandaliwa ripoti ya pamoja itakayokuwa na mapendekezo kuhusu njia za kuboresha hali ya haki za binadamu hapa Ujerumani. Mapendekezo hayo hayana mafungamano, lakini hata hivyo serikali ya Ujerumani itayachunguza kikamilifu. Miaka minne ijayo wakati Ujerumani itakaporudi tena mjini Geneva, baraza la haki za binadamu litatathmini ikiwa serikali ya Ujerumani imezitimiza ahadi zake.