1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawatimua wahalifu wa Afghanistan

30 Agosti 2024

Ujerumani imesema kuwa imewatimua wahalifu wa Afghanistan kurejea nchini mwao kwa mara ya kwanza tangu mamlaka ya Taliban ilipoingia madarakani kimabavu mnamo mwaka 2021.

Maafisa wa polisi wa Ujerumani waweka mashada ya maua kumkumbuka mwenzao aliyeuawa huko Mannheim katika shambulizi la kisu wakati wa mkutano wa kisiasa mnamo Mei 31
Maafisa wa polisi wa Ujerumani waweka mashada ya maua kumkumbuka mwenzao aliyeuawa huko MannheimPicha: Thomas Lohnes/Getty Images

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amewataja raia hao 28 wa Afghanistan kama wahalifu waliopatikana na hatia lakini hakuelezea wazi makosa yao.

Katika taarifa, Hebestreit amesema maslahi ya usalama wa Ujerumani ni muhimu zaidi kuliko madai ya ulinzi wa wahalifu na watu wanaohatarisha usalama wa kitaifa.

Scholz awatahadharisha wahalifu

Akizungumza wakati wa hafla ya kampeini karibu na mji wa Leipzig hii leo, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ameitaja hatua hiyo kuwa ishara ya wazi kwamba wale wanaofanya uhalifu hawawezi kutegemea kwambaUjerumani haitawarudisha makwao na kwamba wanaangazia njia za kufanya hivyo.

Kwa upande wake, waziri wa masuala ya ndani wa Ujerumani Nanc Faeser amesema usalama wa Ujerumani na uongozi wa sheria unachukuwa hatua.

Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: T.Rooks/DW

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani uamuzi huo wa kuwarejesha raia hao wa Afghanistan nchini mwao na kuishtumu Ujerumani kwa mbinu za uchaguzi na kukiuka majukumu yake chini ya sheria za kimataifa.

Mkuu wa shirika hilo nchini Ujerumani Julia Duchrow, amesema hakuna aliye salama nchini Afghanistan na kwamba kwa serikali ya Ujerumani kuwarudisha watu hao nchini humo, inakabiliwa na hatari ya kuwa mshirika wa Taliban.

Soma pia:Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao

Kurejeshwa kwa raia hao wa Afghanistan nchini mwao, kunakuja wiki moja baada ya shambulizi la kisu katika hafla moja mjini Solingenkuishtua Ujerumani huku kundi la itikadi kali linalojiita dola la kiislamu IS likidai kuhusika.

Pia kunakuja kabla ya uchaguzi wa kikanda unaofuatiliwa kwa karibu katika majimbo mawili ya mashariki mwa Ujerumani siku ya Jumapili, ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, kinachopinga uhamiaji cha AfD kinatarajiwa kupata mafanikio makubwa.