1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yazindua mswada wa kuhalalisha bangi

Timothy Jones Iddi Ssessanga
16 Agosti 2023

Rasimu ya mswada ambao utaruhusu kisheria watu kutumia na kukuza bangi inapaswa kuwekwa mbele ya wabunge ili kuzingatiwa. Lakini kuna sauti nyingi zinazopinga kuhalalishwa kwa dawa hiyo kwa madhumuni ya burudani.

Uhalalisahi wa bangi
Rasimu ya mswada wa sheria inafanya kuwa halali kuotesha hadi mimea mitatu ya bangiPicha: Countrypixel/IMAGO

Rasimu ya mswada wenye utata kuhusu kuhalalisha matumizi ya burudani ya bangi ilizinduliwa Jumatano na Waziri wa Afya Karl Lauterbach baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri la Ujerumani.

Watetezi wa matumizi halali ya bangi katika serikali ya muungano ya Ujerumani wanalenga kuhalalisha madawa hayo mwaka huu lakini wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa wabunge wahafidhina, baadhi ya madaktari na wawakilishi wa utekelezaji wa sheria.

Lauterbach aliita rasimu ya muswada huo "hatua ya mabadiliko" kufuatia sera kuhusu bangi ambazo "zimeshindwa kwa bahati mbaya." Hata hivyo, alisisitiza kuwa matumizi ya madawa hayakosi hatari.

"Hakuna anayepaswa kuelewa sheriavibaya. Utumiaji wa bangi utahalalishwa, lakini bado ni hatari," alisema katika taarifa ya pamoja ya Wizara ya Afya na Wizara ya Kilimo.

Soma pia: Afrika kuongoza kwa kilimo cha bangi ya matibabu

Alisema lengo ni kukabiliana na soko la magendo na uhalifu unaohusiana na dawa za kulevya, biashara ya vitu vinavyolewesha au sumu na idadi ya watumiaji.

"Ulinzi wa watoto na vijana ni sehemu kuu ya mradi mzima wa kutunga sheria," ilisema taarifa hiyo, ikirejelea kampeni ya taarifa kwa vijana "Kisheria, lakini ..." ambayo itazinduliwa na Wizara ya Afya.

Ujerumani hushuhudia maandamano ya mara kwa mara kuunga mkono uhalalishaji wa bangi.Picha: TOBIAS SCHWARZ/AFP/Getty Images

Waziri wa Kilimo Cem Özdemir aliita rasimu ya sheria "hatua muhimu kuelekea sera ya maendeleo, yenye msingi wa uhalisia kuhusu dawa za kulevya."

Alisema sheria hiyo "iliyopitwa na wakati" itatumika kuharamisha watu wengi wanaotumia bangi kwa madhumuni ya kibinafsi tu, na kuongeza ulinzi wa watoto na vijana.

Kulingana na takwimu za serikali ya shirikisho, watu wazima milioni 4.5 nchini Ujerumani walitumia bangi angalau mara moja katika mwaka jana.

Rasimu ya muswada inalenga nini?

Rasimu ya sheria hiyo ingefanya kuwa halali kwa watu walio na umri wa zaidi ya miaka 18 kumiliki hadi gramu 25 (wakia 0.9) za bangi na kulima hadi mimea mitatu kwa matumizi ya kibinafsi.

Soma pia:Uganda yasafirisha bangi kwenda Ujerumani 

Kilimo cha hadi mimea mitatu kwa matumizi ya kibinafsi na umiliki wa hadi gramu 25 za bangi kwa madhumuni ya burudani inapaswa kuruhusiwa katika siku zijazo kwa kila mtu mzima.

Pia kutakuwa na uidhinishwaji wa kinachojulikana kama vyama vya kilimo. Vyama hivyo ambavyo aghalabu hujulikana kama "vilabu vya kijamii vya bangi," huwapa wanachama wao bidhaa za bangi zinazozalishwa nyumbani.

Wanachama hawataruhusiwa kutumia bangi kwenye majengo ya vilabu au ndani ya mita 200 kutoka eneo hilo. Vilabu vyenyewe lazima visiwe ndani ya mita 200 kutoka shule, vituo vya kulelea watoto, au shule za chekechea - jambo ambalo litafanya kupata eneo linalofaa kuwa changamoto kubwa.

Waziri wa Afya, Karl Lauterbach (SPD) akipiga picha mbele ya ubao wa kidijitali unaosomeka "bangi ni halali lakini.." akiwasili kwa ajili ya mkutano na waandishi wa habari kuhusu pendekezo la sheria ya kuhalalisha bangi Agosti 16, 2023 mjini Berlin, Ujerumani.Picha: Michele Tantussi/Getty Images

Kuondoa kosa ni hatua ya kwanza. Katika hatua inayofuata, maduka maalum yanaweza kuuza bangi na bidhaa zilizo na THC. Lakini katika wilaya tu na miji iliyochaguliwa, ambayo inapaswa kuitwa mikoa mfano kwa muda wa miaka mitano.

Hapo awali kulikuwa na matarajio makubwa ya mapato ya kodi na kwa akiba katika matumizi ya polisi na mahakama. Lakini makadirio yamesahihishwa na sasa yamewekwa kwa euro laki kadhaa, badala ya mabilioni.

Akiba hiyo inafidiwa na matumizi ya ziada kwa ajili ya tathmini ya sheria pamoja na taarifa na mapendekezo ya kuzuia.

Upinzani dhidi ya mswada kutoka pande zote

Madaktari wamekosoa mapendekezo hayo: Katika taarifa ya pamoja, vyama vitano vya madaktari wa watoto na vijana vimeonya kuhusu "tishio kwa afya ya akili na fursa za maendeleo ya vijana nchini Ujerumani." Muungano wa polisi pia unapinga mswada huo.

Na Chama cha Majaji cha Ujerumani kilionya dhidi ya kazi ya ziada kwa mahakama kwa sababu ya kanuni nyingi za kina juu ya vilabu vya bangi na utoaji wa dawa.

Wabunge wa kihafidhina kutoka majimbo kadhaa pia wamejitokeza kupinga sheria inayopendekezwa. Wanalalamika kuwa mradi huo "siyo wa kuwajibika kitabibu" au wanauonesha kama "shambulio dhidi ya vijana na ulinzi wa afya".

Vijana na uhalalishaji wa bangi

01:08

This browser does not support the video element.

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la mashariki la Saxony, Armin Schuster, wa chama cha upinzani cha Christian Democrats (CDU), alikiambia chumba cha habari cha kampuni ya Redaktionsnetzwerk Deutschland kwamba "sheria hii italeta hasara kamili ya udhibiti."

Soma pia: Rwanda yaruhusu bangi itumike kimatibabu na kiuchumi

"Kama kuna kitu ambacho hatuhitaji, basi ni sheria hii," waziri wa mambo ya ndani wa jiji la Hamburg, Andy Grote, kutoka chama cha mrengo wa kushoto cha Lauterbach cha Social Democrats (SPD) aliliambia shirika la utangazaji la umma NDR. "Uzoefu kutoka nchi nyingine unaonyesha kuwa kuhalalisha kunasababisha ongezeko kubwa la matumizi, pamoja na hatari na athari zake," alisema.

Grote pia alitilia shaka iwapo kuhalalishwa kwa matumizi ya burudani ya bangi kungesababisha kupunguzwa kwa biashara ya soko la magendo kama inavyodaiwa mara nyingi na watetezi wa hatua hiyo.

"Inastahili kuhofiwa kwamba bangi haramu itahitajika sana kwa sababu ya uwezo wake wa juu na bei nafuu na kwamba soko la magendo na soko halali litachanganywa pamoja," alisema.

Grote pia alisema udhibiti wa matumizi ya bangi utahitaji "urasimu wa kina wa ufuatiliaji wa bangi" ili kuhakikisha kuwa masharti yake yote yanazingatiwa.

Hata wabunge kutoka chama mshirika wa muungano wa Lauterbach cha  Free Democrats (FDP), ambao kimsingi wanaidhinisha uhalalishaji huo wanazungumza juu ya "jitu la ukiritimba".

Watetezi wa uhalalishaji pia hawajaridhika. Wanasema kanuni mpya zina maelezo mengi na haziendi mbali vya kutosha.

Waziri wa Afya Lauterbach hajafadhaika. Anachukulia ukosoaji kutoka pande zote mbili kuwa ishara nzuri na anazungumza juu ya "sheria yenye hisia ya uwiano".

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW