Ujumbe wa Eritrea wawasili Ethiopia kwa mazungumzo
26 Juni 2018Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameupokea ujumbe kutoka Eritrea unaofanya ziara ya kwanza ya ngazi ya juu nchini humo baada ya takriban miongo miwili. Ziara hiyo imeibua matumaini ya kumalizika kwa mojawapo ya mikwamo ya muda mrefu zaidi ya kijeshi barani Afrika.
Wanariadha wa michezo ya Olimpiki wa Ethiopia, waimbaji, waigizaji na viongozi wa kidini pia walikuwapo katika uwanja wa ndege ambapo Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Eritrea Osman Saleh na maafisa wengine wakuu walipokelewa kwa mashada ya maua huku bendera za nchi zote mbili zikipepea katika mji wa Addis Ababa na mabango yenye ujumbe wa "Karibu!" yakitundikwa katika milingoti ya taa za barabara za mji huo.
Masharti ya makubaliano ya amani ya 1998-2000 yataheshimiwa?
Ziara ya leo Jumanne, inajiri baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kusema mwezi huu kuwa angetaka kuheshimu masharti yote ya makubaliano ya amani ya mwaka 1998-2000 baina ya nchi hizo mbili jirani, katika ishara ya utayarifu wake kumaliza mzozo wa mpaka baina ya nchi hizo mbili.
Idhaa ya Kiingereza ya DW imemhoji mwandishi mkongwe wa habari na vitabu Michela Wrong ambaye kwa miaka mingi amekuwa akifuatilia matukio ya Ethiopia na Eritrea kuhusu umuhimu wa ziara hii na amesema: "Huu ni wakati wa ufanisi, ni ujumbe wa ngazi ya juu sana. Waziri Mkuu wa Ethiopia alifikia hatua ya kuwasilisha ujumbe wa maridhiano kwa Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, ambayo ni ishara muhimu wa maridhiano na urafiki. Kwa hivyo ishara zinaonekana kuwa nzuri, na bila shaka huu ni mkutano muhimu”
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki aliukaribisha ujumbe chanya wa Ethiopia na akaamua kutuma ujumbe ambao umemjumuisha mshauri wake Yemane Gebreab na mjumbe wake katika Umoja wa Afrika. Hayo ni kwa mujibu wa aliyewashuhudia wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Bole.
Matarajio ya kumaliza mzozo wa miaka 20
Eritrea ilipata uhuru wake kutoka Ethiopia mwaka 1993 baada ya miongo mitatu ya vita vya ukombozi. Lakini vita vilizuka tena baina yao mwaka 1998 kuhusu mpaka unaozozaniwa, na tangu wakati huo uhusiano wao wa kidiplomasia ulivunjika.
Mkuu wa shughuli za ofisi ya Abiy aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa waziri mkuu anatarajia ziara hiyo itaweka msingi wa mustakabali mwema kwa Ethiopia na Eritrea.
Vita vya mzozo wa mpaka vilisababisha vifo vya watu 80,000, na pande zote zimekuwa zikitofautiana kuhusu uliko mji wa mpakani wa Badme huku mpaka huo ukisimamiwa na majeshi.
Eritrea na Ethiopia zilivunja uhusiano wao wa kidiplomasia miaka 20 iliyopita japo Eritrea ina ujumbe wa kudumu mjini Addis Ababa unaoiwakilisha katika makao makuu ya Umoja wa Afrika.
Hakuna wawakilishi wa Eritrea ambao wamewahi kuwa sehemu ya mazungumzo rasmi na serikali ya Ethiopia tangu mwaka 1998.
Mwandishi: John Juma/Ap/RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga