Ujumbe wa Hamas wawasili Cairo
7 Machi 2025
Maafisa wawili waandamizi wa kundi hilo la Kipalestina, wamesema Ijumaa kuwa ujumbe huo utakutana na maafisa wa Misri Jumamosi kujadiliana hatua zilizopigwa hivi karibuni, kutathmini maendeleo katika kuyatekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano na kuzungumzia masuala yanayohusiana na kuanzisha awamu ya pili ya mpango wa kusitisha mapigano.
Mmoja wa maafisa hao ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa katika mkutano huo na wapatanishi wa Misri, Hamas itaiomba Israel kutekeleza makubaliano, kuanza awamu ya pili ya mazungumzo, na kufungua vivuko kwenye maeneo ya mpakani ili kuruhusu msaada kuingia katika Ukanda wa Gaza.
Amesema katika awamu ya pili ya makubaliano, Hamas inataka Israel iondoke kabisa Gaza, na kumaliza mzingiro, ujenzi mpya wa Gaza na msaada wa kifedha kwa kuzingatia maamuzi ya mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa ya Kiarabu uliofanyika wiki hii mjini Cairo. Kulingana na afisa huyo, Hamas iko tayari kujadiliana kuhusu kubadilishana wafungwa ili kuwaachilia huru mateka wote wa Israel wakiwemo raia wa Marekani.
Siku ya Jumatano Rais wa Marekani Donald Trump aliwaonya watu wa Gaza kuwa wataangamizwa, ikiwa mateka wote wanaoendelea kushikiliwa na Hamas hawatoachiwa sasa. Inaaminika kuwa raia watano wa Marekani ni miongoni mwa wanaoendelea kushikiliwa mateka. Wanne wamethibitishwa kufariki na mmoja Edan Alexander, anaaminika bado yuko hai.
Ujerumani yaunga mkono mpango wa nchi za Kiarabu
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesema leo kuwa nchi hiyo inaunga mkono mpango uliowasilishwa na mataifa ya Kiarabu kuhusu ujenzi mpya wa Gaza, ambao kwa kiasi kikubwa uliandaliwa Misri.
''Mpango huo una vipengele vingi vizuri ambavyo vinaweza kutumika kama msingi wa kupata mafanikio zaidi na mazungumzo yenye kujenga kuhusu mpango huu yanapaswa kuanza sasa. Ni muhimu sana kwa serikali ya Ujerumani kwamba Gaza sio kitisho tena kwa Israel,'' alisisitiza Hebestreit.
Aidha, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani Sebastian Fischer ameongeza kusema kuwa Ujerumani itajadili kwa ukaribu zaidi taarifa hizo na washirika wake wa Magharibi na wa mataifa ya Kiarabu. Kulingana na Fischer, nchi za Kiarabu zimeonyesha ishara muhimu ambayo inaashiria nia yao ya kutoa mchango wao katika kupata suluhisho endelevu kwenye mzozo wa Gaza.
Mkutano wa Geneva kuhusu raia wa Palestina wafutwa
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi imesema kuwa mkutano uliokuwa ufanyike Geneva kujadiliana kuhusu kuwalinda raia kwenye maeneo ya Kipalestina yanayokaliwa kimabavu na Israel umefutwa baada ya nchi chache tu kati ya 196 kukubali mwaliko wa kuhudhuria.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuitaka Uswisi kuitisha mkutano huo ili kuthibitisha tena Makubaliano ya Geneva, msingi wa sheria za kimataifa za kibinaadamu, kutokana na wasiwasi kwa Wapalestina. Israel imeukosoa mkutano huo ikiutaja kama ''sehemu ya matumizi ya mifumo ya kisheria'' dhidi ya nchi hiyo.
(DPA, AFP, AP, Reuters)