1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Ujumbe wa Iran wazuru Saudia kusawazisha mahusiano

12 Aprili 2023

Ujumbe wa Iran umewasili nchini Saudi Arabia kufungua njia ya kuanzishwa tena kwa uhusiano wa kibalozi wakati mataifa hayo hasimu yakijiandaa kurejesha uhusiano wao kuwa wa kawaida miaka saba baada ya kutengana.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser kanani, amesema kulingana na utekelezaji wa makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia kuhusu kuanzishwa tena kwa shughuli za kidiplomasia, jopo la kiufundi la Iran liliwasili mjini Riyadh leo mchana na kukaribishwa na maafisa wa nchi hiyo.

Katika taarifa, Nasser amesema kuwa ujumbe huo wa Iran utachukuwa hatua zinazohitajika kufungua tena ubalozi mjini Riyadh na ubalozi mdogo mjini Jeddah pamoja na shughuli za mwakilishi wa kudumu wa Iran katika shirika la Ushirikiano wa Kiislamu lenye makao yake Jeddah.