1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa kupambana na Ebola kufungwa baada ya mapambano

21 Desemba 2014

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na Ebola utafungwa haraka mara mapambano dhidi ya ugonjwa huo yatakapofanikiwa, katibu mkuu Ban Ki-moon amesema Jumamosi (20.12.2014) wakati wa ziara yake katika Afrika magharibi.

Ban Ki-moon in Liberia 19.12.2014
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-moon akifanyiwa uchunguzi wa afya yake LiberiaPicha: Reuters/J. Giahyue

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na dharura ya ugonjwa wa Ebola, UNMEER, uliundwa mwezi wa Septemba mwaka huu kuratibu sera na mipango ya kampeni ambayo inajumuisha serikali, mashirika ya kutoa misaada na wafanyakazi wa huduma ya afya kutoka mataifa hayo yaliyoathirika.

Ban amesema UNMEER ni tofauti na ujumbe wa kulinda amani na ujumbe huo haupaswi kuendelea kupindukia wajibu wake wa wakati huu.

Ban Ki-moon akiwa nchini GhanaPicha: picture-alliance/epa/E. Schneider

"Kuna mazoea kwamba ujumbe unaendelea kutokana na hali isiyo thabiti ya kisiasa na mizozo. Ebola ni ugonjwa wa dharura na usiotabirika, kwahiyo hatuwezi kuchukua muda mrefu wa kuutokomeza," ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Ndio sababu natoa ujumbe wa kisiasa. Sio kwamba tumefikia uamuzi wowote juu ya lini UNMEER itafikia mwisho, lakini unapaswa kuwa ujumbe wa muda mfupi," amesema.

Zaidi ya watu 7,300 wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola katika mataifa matatu ambayo yameathirika mno na ugonjwa huo, Liberia, Sierra Leone na Guinea. Ban amekataa kutaja siku ya kuumaliza ugonjwa huo, lakini amesema anatiwa moyo kwamba kiwango cha maambukizi mapya kinapungua.

Umuhimu wa mapambano

Ametembelea vituo vya kutibu wagonjwa katika nchi hizo zilizoathirika na ugonjwa huo wakati wa ziara yake ya saa 36 kuonesha umuhimu wa mapambano dhidi ya virusi hivyo na kuwatia moyo wafanyakazi wa afya.

Ban Ki-moon akiwasili nchini LiberiaPicha: Reuters/J. Giahyue

Jumamosi (20.12.2014) alikutana pia na Ibrahim Boubacar Keita, rais wa Mali, nchi ambayo hivi karibuni ilishuhudia mgonjwa wa mwisho kati ya wagonjwa wanane wa mwisho wa Ebola akiruhusiwa kutoka Hospitali.

Kila mahali alipotembelea, maafisa wa afya walichukua vipimo vya joto la mwili wake na kuhakikisha anasafisha mikono kwa maji yaliyotiwa dawa ya klorini katika ishara kwamba hakuna mtu anaweza kuachiwa bila ya kupitia hatua za usalama.

Nchini Guinea Ban amezihimiza nchi kuepuka kuwatenga wafanyakazi wa afya wanaopambana dhidi ya ugonjwa huo wa Ebola.

Shujaa Rebecca Johnson

Matamshi yake yanafuatia mkutano katika kituo cha matibabu nchini Sierra Leone siku ya Ijumaa ambapo Rebecca Johnson, muuguzi anayewatibu wagonjwa, alielezea jinsi alivyopatwa na ugonjwa huo, akapona na sasa amerejea kuwatibu wagonjwa wa Ebola.

Ban alimkumbatia hadharani Johnson na mara kadhaa alimtaja kuwa mfano wa ushujaa, mbali ya kwamba amesema mpaka sasa anakabiliwa na hali ya kutengwa kama mtu aliyenusurika na ugonjwa huo.

Wakati huo huo Waliberia wamepiga kura Jumamosi (20.12.2014) katika uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu wa baraza la Seneti katika nchi hiyo iliyoathirika na ugonjwa wa Ebola wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akikamilisha ziara yake wa kutathimini mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre

Mhariri: Elizabeth Shoo.