1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Saudia wawasili Uturuki kuhusu suala la Khashoggi

13 Oktoba 2018

Saudi Arabia imepinga Jumamosi tuhuma kwamba Jamal Kashoggi aliamriwa kuuliwa na kikosi cha mauji ndani ya ubalozi wake mdogo wa Istanbul, na kusema tuhuma hizo hazina msingi. Kadhia hiyo imevutia nadhari ya kimataifa.

Jamal Khashoggi saudischer Journalist
Picha: picture-alliance/dpa/H. Jamali

Huku utata ukiongezeka kuhusu hatma ya mwandishi huyo wa habari na mkosoaji wa utawala mjini Riyadhi, gazeti la Washington Post liripoti kuwa limepata sauti zilizorekodiwa ndani ya jengo zinazodaiwa kuthibitisha madai yao kwamba Kashoggi aliteswa na kuuawa katika ofisi ya ubalozi.

Ujumbe wa Saudi Arabia uliwasili nchini Uturuki kwa mazungumzo, maafisa walisema siku ya Ijumaa, huku kadhia hiyo ikizidi kuuweka mashakani uhusiano tete kati ya mataifa hayo.

Katika majibu ya kwanza yaliotolewa na wizara ya Saudi Arabia kuhusu tuhuma za mauaji ya Kashoggi, waziri wa mambo ya ndani Mwanamfalme Abdel Aziz bin Saud bin Nayef alisema kwamba "kilichokuwa kinaenezwa kuhusu maagizo ya kumuua ni uongo na madai yasio na msingi."

Falme "imejifunga kuheshimu kanuni zake, sheria na tamaduni na inaheshimu sheria na mikataba ya kimataifa," aliongeza kusema kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la serikali ya Saudi Arabia SPA.

Kadhia hiyo inahatarisha kuharibu sifa ya Saudi Arabia na uhusiano wake na mataifa ya Magharibi wakati ambapo mrithi wa kiti cha ufalme mwanamfalme Mohammed bin Salman akipigia chapuo kampeni yake ya mageuzi nyumbani.

Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul ambako Khashoggi alionekana akiingia mara ya mwisho kabla ya kutoweka.Picha: picture-alliance/AA/A. Bolat

Majina makubwa katika sekta ya habari na biashara tayari yamefuta ushiriki wao katika wa mkutano mkubwa wa uwekezaji uliopangiwa kufanyika mjini Riyadhi mwezi ujao.

Saudi Arabia yakanusha kuhusika

Kashoggi, mwandishi habari wa Kisaudi na mchangiaji wa gazeti la Washington Post alitoweka Oktoba 2 baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia kupata nyaraka za kumuwezesha kuoa. Duru za serikali ya Uturuki zinasema polisi wanaamini aliuawa lakini Riyadh inakanusha hayo.

Ujumbe wa Saudi, ambao muundo wake haukubainika mara moja, unatarajiwa kukutana na maafisa wa Uturuki mjini Ankara mwishoni mwa wiki, vimeripoti vyombo vya habari vya serikali siku ya Ijumaa.

Kuna uwezekano kwamba watashiriki katika kikosi kazi cha pamoja kuhusu kesi hiyo, ambacho kuundwa kwake kulitangazwa na msemaji wa rais Ibrahim Kalin kufuatia maombi ya Saudi Arabia.

Afisa wa serikali ya Saudi Arabia alienukuliwa na shirika la habari la SPA alisema ilikuwa "hatua chanya" kwa Uturuki kukubali kuunda kile kinachoelezwa kuwa "timu ya pamoja" kuhusiana na kutoweka kwa Khashoggi.

Uturuki yasita kuitumu Saudi Arabia

Mpaka sasa serikali ya Uturuki imejizuwia kuituhumu Saudi Arabia, ingawa vyombo vya habari vinavyoelemea serikali vimechapisha madai ya mihemko, yakiwemo kwamba "timu ya mauji" ilitumwa mjini Istanbul kumuuwa Khashoggi.

Katika matamshi ya nadra ya wazi kuhusu kadhia hiyo iliyotolewa na afisa wa serikali, balozi wa Saudi Arabia nchini Uingereza, Mwanamfalme Mohammed bin Nawaf al Saud, aliiambia BBC kwamba Riyadh ilikuwa na wasiwasi kuhusu raia wake.

Rais wa Uturuki Recep Tayyio Erdogan ameitaka Saudi Arabia kutoa picha za CCTV kuthibisha maelezo yake kwamba Khashoggi aliondoka kwenye ofisi hiyo ya ubalozi akiwa salama.

Khashoggi, raia wa Saudi anaeishi nchini Marekani tangu Septemba 2017 akihofia kukamatwa, alikosoa baadhi ya sera ya mwanamfalme Mohammed bin Salman na uingiliaji wa Riyadh katika vita nchini Yemen.

Mwanachama wa chama cha haki za biandamu - tawi la Istanbul akibeba picha ya Khashoggi mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Picha: picture-alliance/AA/O. Coban

Gazeti la Washington Post liliripoti kuwa serikali ya Uturuki imewaambia maafisa wa Marekani kuwa inao mkanda wa sauti na vidio vinavyoonyesha namna Khashoggi "alivyohojiwa, kuteswa na kisha kuuawa" ndani ya ofisi ya ubalozi kabla ya mwili wake kukatwa vipande. Maafisa wa Uturuki walioulizwa na shirika la habari la AFP walikataa kuzungumzia ukweli wa ripoti hiyo.

Uhusiano kati ya Ankara na Riyadh

Ankara na Riyadh zimekuwa zikisimama pande kinzani kuhusu masuala muhimu ya kikanda, ikiwemo kupinduliwa kwa serikali ya Udugu wa Kiislamu nchini Misri na hatua ya mwaka uliopita ya kuiwekea vikwazo na vizuwizi mshirika wa Uturuki Qatar, iliyoongozwa na Saudi Arabia. Lakini licha ya hayo, kama dola muhimu za Kisunni zimeeendeleza uhusiano mzuri baina yao.

Lakini licha ya kukubali kwa Riyadhi Jumanne kuwaruhusu maafisa wa Uturuki kupekua ofisi yake ya ubalozi, upekuzi huo bado haujafanyika. Pande hizo mbili zimekuwa na mawasiliano mazito kujaribu kutatua suala hilo, vimeripoti vyombo vya habari vya ndani.

Gazeti linaloelemea serikali ya Uturuki la Sabah lilisema upekuzi wa ubalozi huo mdogo haujafanyika kwa sababu maafisa wa Saudi Arabia walitaka kuruhusu uchunguzi wa juujuu tu.

Upande wa Uturuki haukukubaliana na pendekezo hilo na gazeti la Sabah lilisema maafisa walitaka kupekuwa jengo hilo kwa kutumia kemikali ya luminol, ambayo inaruhusu timu za uchunguzi wa makosa ya jinai kugundua dalili za damu.

Maafia walikuwa wanachunguza rekodi za sauti zilizotumwa kutoka saa ya kisasa ambayo Khashoggi alikuwa amevaa wakati alipoingia ubalozini kwenda kwenye simu ya smart aliompa mchumba wake wa Kituruki aliekuwa anamsubiria nje, Hatice Cengiz.

Gazeti la kila siku la Milliyet liliripoti kwamba "malumbano na kelele" vilikuwa vikisikika kwenye rekodi hizo, lakini gazeti la Sozcu lilisema kwamba "baadhi tu ya sauti ndiyo zilikuwa zisikikika.

Mchumba wa Khashoggi Hatice (kushoto) akiwa na marafiki zake wakimsubiri mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Oktoba 3, 2018.Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Mkutano wa uwekezaji wasusiwa

Makampuni ya Bloomberg, Financial Times, The Economist na The New York Times yaljitoa kuwa wafadhili wa habari kwenye mkutano wa pili wa Uwekezaji wa Baadae unaotarajiwa kufanyika kati ya Oktoba 23-25 mjini Riyadh uliopewa jina la "Davos Jangwani" baada ya jukwaa la kimataifa ya kiuchumi katika eneo la mapunziko nchini Uswisi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya usafirishaji ya Uber, Dara Khosrowshahi, alisema hatohudhuria tena mkutano huo hadi pale "ukweli mweingine tofauti na wa sasa utakapotolewa."

Mjasiliamali wa Kiingereza Richard Brandson alisema atasitisha ukurugenzi wake unaohusiana na miradi miwili ya utalii nchini Saudi Arabia, kuhusiana na wasiwasi kuhusu mwandishi huyo alietoweka.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Saudi Arabia kueleza kilichomsibu Khashoggi, likisema Riyadh ilikuwa inawajibika kwa uchache kutokana na kutoweka kwa laazima.

     

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri: Isaac Gamba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW