1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi na uchunguzi wa ukiukaji wa haki unahitajika Sudan

21 Juni 2024

Umoja wa Afrika, AU, umeombwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kupeleka ujumbe wa ulinzi wa kiraia ili kukabiliana na ukatili unaoendelea nchini Sudan, huku ripoti za vifo, njaa na watu kuhamishwa zikitolewa.

Wakimbizi wa Sudan katika mji unaokabiliwa na mapigano wa El Fasher, 14, Juni 2024.
Wakimbizi wa Sudan katika mji unaokabiliwa na mapigano wa El Fasher, 14, Juni 2024.Picha: DW

Umoja wa Afrika, AU, umeombwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kupeleka ujumbe wa ulinzi wa kiraia ili kukabiliana na ukatili unaoendelea nchini Sudan, na kuchukua hatua kuhakikisha uchunguzi thabiti wa haki za binadamu umefanyika.

Kwa mujibu wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch mamia ya raia wameuawa na pande zinazopigana Sudan katika mashambulizi ya hivi karibuni huko El Fasher kaskazini mwa Darfur.

Nchi wanachama wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, PSC wanaokutana tarehe 21 Juni, 2024 wamehimizwa kujitolea kuchukua hatua madhubuti za kuwaweka raia salama na kuhakikisha uwajibikaji wakati hatari ya ukatili zaidi dhidi ya raia katika eneo la El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, na migogoro mingine kwenye maeneo yaliyoathirika nchini humo yanaendelea kuongezeka.

Soma pia: Baraza la usalama la umoja wa mataifa lataka kusitishwa kwa mzingiro El-Fasher

Raia wa Darfur wanahitaji ulinzi

Allan Ngari, mkurugenzi wa utetezi wa Afrika katika shirika la Human Rights Watch anasema, "ombi la hivi karibuni la baraza hilo, la kuyataka mashirika mengine ya Umoja wa Afrika kuchukua hatua, ni hatua nzuri iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya kushughulikia hali ya Sudan ambayo ni moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani".

Mkutano wa wakuu wa nchi wa Juni 21 unafanyika huku vita vya kutisha kati ya Jeshi la Sudan, SAF na vikosi vya wanamgambo wa RSF na washirika wao sasa vimedumu kwa miezi 14.

Picha iliyopigwa Januari 2024, inaonyesha wanawake na watoto wachanga katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam, karibu na El Fasher huko Darfur Kaskazini, SudanPicha: Mohamed Zakaria/REUTERS

Anapendekeza kwamba, "katika mkutano wake wa ijumaa, baraza hilo la Umoja wa Afrika linapaswa kueleza ni hatua gani za dharura linapanga kuchukua ili kuhakikisha kutumwa kwa ujumbe wa ulinzi wa raia unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kusaidia uchunguzi wa Tume ya Afrika kuhusu haki za binadamu.”

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya makundi yanayopigana ya Sudan eneo la El Fasher kaskazini mwa Darfur yamewaua mamia ya raia na kuwalazimisha maelfu kuyakimbia makazi yao, huku maelfu ya watu ndani na nje ya eneo hilo wakikabiliwa na njaa.

Hitaji la msaada wa kibinadamu laongezeka

Pande zote mbili zimehusika na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuzuia misaada na unyanyasaji wa kijinsia.

Mapigano huko El Fasher kati ya pande hizo mbili yaliongezeka katikati ya mwezi Mei mwaka huu. Shirika la Médecins Sans Frontières, madaktari wasio na mipaka limesema kuwa Hospitali ya Kusini, kituo pekee cha huduma za dharura cha jiji hilo, na baadaye hospitali ya Saudi ilipokea majeruhi 1,418 kati ya mwezi Mei 10 na mwezi Juni 11, mwaka huu; na 226 kati yao walifariki. Wengine wengi hawakuweza kufika hospitalini.

Soma pia: Msaada wa chakula waongezeka Darfur lakini hautoshi - WFP

Mnamo Juni 8, wanamgambo wa RSF waliishambulia Hospitali ya Kusini. Wapiganaji waliingia hospitalini wakiwapiga risasi, hatua iliyowalazimu wagonjwa, jamaa zao na wafanyikazi wa matibabu kukimbia na kwenda sehemu salama.

Afisa wa Wizara ya Afya alisema RSF ilimpiga yeye na madaktari wengine wawili wakati wa tukio hilo. Kundi hilo pia lilipora vifaa vya matibabu na hatimaye hospitali ililazimika kufungwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW