1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa usalama wa UN washambuliwa Douma

18 Aprili 2018

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kuandaa usalama wa timu ya wakaguzi wa OPCW chashambuliwa kwa risasi mjini Douma na kusababisha mashaka juu ya ziara ya timu ya wakaguzi hao wa kimataifa

Syrien UN-OPCW
Picha: Reuters/O. Sanadiki

Ujumbe wa usalama wa Umoja wa Mataifa umeshambuliwa wakati ukiwa katika operesheni yao maalum nchini Syria katika mji wa Douma ya kuandaa mazingira ya kupelekwa  wataalamu wa kuchunguza madai ya kutumiwa silaha za sumu katika shambulizi lililouwa raia kadhaa nchini Syria,hivi karibuni.Taarifa zilizotolewa na afisa mmoja wa kutoka Umoja huo wa Mataifa zinasema kwamba risasi zilifyetuliwa dhidi ya timu ya Umoja huo mjini Douma lakini hakuna aliyejeruhiwa na wote wamerejea mjini Damascus. Haijulikani ni lini ujumbe wa shirika la OPCW utakwenda Douma.

Balozi wa Uingereza katika shirika la Kimataifa la kudhibiti silaha za sumu  OPCW Peter Wilson amewaambia waandishi habari kwamba safari ya kuelekea Douma ya  kundi la wakaguzi wake imecheleweshwa  baada ya kutokea shambulio dhidi ya timu ya walaamu wa hatua ya awali ya ukaguzi kutoka kitengo kinachoshughulika na usalama cha Umoja wa Mataifa huko Douma ambayo imelazimika kujiondoa katika mji huo.

Picha: picture-alliance/Photoshot

Balozi Peter Wilson ameyanukuu maelezo aliyopewa na mkurugenzi mkuu mtendaji wa OPCW Ahmet Üzumcu. Awali duru za kidiplomasia zililiambia shirika la habari la Reuters kwamba Üzümcu amesema wakati wanajeshi wa  Umoja wa Mataifa wa kuandaa mazingira ya kiusalama kwa ajili ya kundi la waataalamu wa OPCW walipowasili katika mji wa Douma jana Jumanne  kundi kubwa la watu walijitokeza.

Na punde walipokwenda kuatazama mojawapo ya eneo yalikotokea mashambulio yanayodaiwa kuwa ya silaha za sumu walianza kufyetuliwa risasi na mabomu madogo madogo na ndipo walipoondoka katika eneo hilo. Kutokana na hali hiyo ujumbe wa kutafuta ukweli wa kile kilichotokea Douma hauwezi kuondoka kuelekea katika mji huo wa Syria hadi pale utakapopewa maelekezo ya kufanya hivyo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Ahmet Uzümcü mkuu wa OPCW amewaambia mabalozi mjini The Hague kwamba haijafahamika ni lini timu yake iliyoko mjini Damascus kwa sasa itaondoka kwenda Douma. Timu ya wataalamu wa OPCW iliwasili Damascus tangu Jumamosi wakati Uingereza Ufaransa na Marekani zilipoanzisha hatua za kijeshi dhidi ya kile ilichosema kushambulia maeneo yanayohusishwa na mpango wa silaha za sumu za Syria.

Bashar al-Jaafari-Balozi wa Syria katika Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/AA/M. Elshamy

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jaafari jana alisema kwamba wataalamu wa OPCW wataanza uchunguzi wao mara tu watakapopata muongozo kutoka timu ya kikosi cha usalama cha Umoja wa Mataifa.Lakini pia alisisitiza kwamba serikali ya Syria imefanya kila iwezalo kuratibu shughuli ya ujumbe huo na kilichobaki ni Umoja wa Mataifa wenyewe na OPCW kuamua kupeleka wachunguzi Douma au la.

''Serikali ya Syria imefanya kila kitu ilichoweza kukifanya kuratibu shughuli ya ujumbe huo.Na zaidi ya hilo ujumbe huu umeshaanza kazi tangu ulipowasili Damascus.Jana ulisikiliza taarifa za mashahidi kadhaa kuhusu tukio linalodaiwa silaha za sumu zilitumika.Kwahivyo ujumbe huo umeshaanza kazi na haya yote yanayoelezwa ni porojo. Tetesi zote hizi ni habari za uongo zinazolenga kuvuruga juhudi za kujulikana ukweli na kuhakikisha kwamba watu wanasahaulishwa ile hatua ya matumizi ya nguvu iliyochukuliwa''

Taarifa nyingine zinatangazwa na shirika la habari la Syria zinasema kwamba waasi katika mji wa Kaskazini Mashariki wa Damascus wanasalimisha silaha zao kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya nchi hiyo. Kituo cha televisheni cha Al-Ikhbariya kinasema wapiganaji wa kundi linalojiita  jeshi la waasi wa kiislamu pamoja na familia zao wameanza kuondoka katika mji wa Dumayr ulioko karibu na Ghouta Mashariki.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW