1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukame wasababisha wafugaji Marsabit kupata hasara

22 Februari 2023

Wafugaji kutoka jimbo la Marsabit nchini Kenya wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa kutokana na makali ya kiangazi ambayo yanashuhudiwa kwenye eneo hilo.

Kenia Marsabit Dürre  Dromedar
Picha: Michael Kwena/DW

Wengi wa wafugaji kwa wakati huu, wameanza kuipiga mnada mifugo yao ambayo imekosa soko kutokana na kudhoofika, huku wengine wakilazimika kwenda mjini Marsabit kutafuta wateja wanaoweza kuinunua mifugo hiyo hata kwa bei ya chini kabisa ili wajikimu kimaisha. 

Mmoja wa wafugaji wa Marsabit Abdiraman Dima, anasema athari ya kiangazi na ukame wa muda mrefu inaonekana waziwazi katika jimbo hilo na hivyo kukosa pesa ya kununua chakula na kilichosalia kwa sasa ni kuiuza mifugo yao kwa bei yoyote ile iwayo, kama anavyo.

Ngamia katika kijiji cha Parapul, Marsabit, kaskazini ya KenyaPicha: Simon Maina/AFP

"Tunahofia kwamba watu huenda wakaanza kuangamia kutokana na makali ya njaa. Watu wanakuja mjini kutoka mbali na wana njaa sana. Zamani ngamia alikuwa anauzwa shilingi 80,000 za Kenya, ila leo ngamia anauzwa shilingi 6,000 tu," alifafanua Dima.

Kwa upande mwengine, hali ngumu ya maisha kwa jamii ya wafugaji imesababisha idadi kubwa ya wanafunzi kubakia nyumbani kutokana na ukosefu wa karo.

Takwimu kutoka idara ya elimu zinaeleza kuwa asilimia 13 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE, 2022 hawajajiunga na shule za sekondari katika jimbo hilo.

Serikali yatakiwa kuwasaidia wanafunzi

Wafugaji wengi sasa wanatoa wito kwa serikali ya kitaifa na ya kaunti kuwasaidia wanafunzi kutoka familia zinazotegemea mifugo ili wajiunge na shule za sekondari kwani mifugo mingi imeangamia kutokana na makali ya ukame.

"Kila wakati mnatuambia tulete karo ya wanafunzi. Sisi hatuna pesa mnaweza kutuuza basi. Serikali itupe chakula kwa sababu mifugo yetu imeangamia yote," alisisitiza Fariah Bulo, mzazi kutoka mji wa Saku.

Wanawake wakipokea msaada wa chakula huko Marsabit, KenyaPicha: Michael Kwena/DW

Kaimu kamishna wa jimbo la Marsabit, David Saruni, amesema serikali imekuwa ikitoa msaada wa chakula kwa wakaazi walioathirika na makali ya ukame japo amedokeza kuwa hali ya ukame inaendelea kuwa mbaya.

Saruni amewahimiza wafugaji kuiuza mifugo yao ili kujipunguzia hasara kutokana na maafa ya mifugo inayoripotiwa. ''Kuna mifugo ambayo imeendelea kudhoofika kwa sababu ya kukosa lishe na kwa sababu ya ukame. Serikali inashirikiana na mashirika kuleta chakula kwa binaadamu na hata mifugo," alisema Saruni.

Jimbo la Marsabit linashuhudia hali mbaya ya ukame, ambao umekuwa kitisho kikubwa kwa maisha ya mifugo waliosalia huku binaadamu wakianza kuwa na hofu kuhusu afya zao.

(DW)
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW